Rais Samia atoa onyo kali kwa wapigaji fedha za miradi ya maendeleo

NA FRESHA KINASA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere katika Kata ya Kwangwa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Ambapo amesisitiza kuwa, Serikali inafuatilia kwa karibu fedha inazozitoa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo zilete tija na kwamba wanaofuja fedha hizo lazima wachukuliwe hatua.

Ameyasema hayo leo Februari 6, 2022 wakati akizungumza na wananchi katika eneo la hospitali hiyo, ambapo amesema kwamba, miradi mingi imekuwa ikisuasua kukamilika kutokana na kupewa wakandarasi wasio na uwezo wa kumudu kuitekeleza na hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi kuvunja mikataba na wakandarasi wasio na uwezo kwa kufuata taratibu zote za kisheria.

Aidha, Mheshimiwa Rais Samia ameonesha kusikitishwa kutokana na miradi mingi kutokuwa na matokeo chanya mkoani Mara, ambapo ameutaka uongozi wa mkoa  na wilaya za mkoa huo kujitathmini katika utendaji kazi wao ambao umekuwa ukikwamisha huduma kwa wananchi na amemsisitiza Mkuu wa Mkoa kutoogopa kufanya maamuzi pale anapoona mambo hayaendi sawia. 

Aidha, Mheshimiwa Rais amewataka wananchi waliopo maeneo ambayo shughuli za uwekezaji, waache kasumba ya tegesha na kuwafanyia fujo wathamini wanapofika maeneo husika kwani yanakwamisha maendeleo ya nchi. Huku Mpango wa kujenga VETA nchi nzima akisema Serikali inafanyiwa kazi ili kusaidia vijana kuondokana na tatizo la ajira.

Amewataka pia viongozi wa Mkoa wa Mara kuacha tabia ya ubinafsi badala yake washughulikie matatizo ya wananchi kwa uzalendo badala ya kusubiria viongozi wakiwemo mawaziri jambo ambalo linaufanya mkoa usifanye vizuri kimaendeleo.

Kwa upande Wake Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema Rais Samia  anagusa maisha ya Watanzania kikamilifu ambapo kwa kipindi cha miezi tisa ya uongozi wake vituo vya afya 233 nchini  vimejengwa  na katika Mkoa wa Mara vituo vya afya  10 vinajengwa.

Ameongeza kuwa,  Rais Samia pia ametoa fedha za ujenzi wa hospitali sita za rufaa za mikoa  pamoja na kutoa fedha za ujenzi wa hospitali  za  kanda  na fedha za dawa alizotoa  Shilingi zaidi ya bilioni 333.8 za madawa. Huku akibainisha kwamba Serikali imeridhia ombi la kuanzisha chuo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ambapo hatua zitafanyika kama ni kujenga chuo cha kati au tawi la MOI kuwezesha kupata madaktari bingwa wabobezi wa mifupa.

Waziri Ummy amewataka Watanzania kujiunga na bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi wanapougua huku akisisitiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kuchanja.

Aidha, Waziri Ummy amesema hajaridhishwa na  hali ya dawa katika vituo vya afya ambapo  wataalamu wanasema upatikanaji wa dawa ni asilimia 90, lakini jambo la kushangaza   wananchi hawapati dawa wanapofika vituo vya afya  huku akiwahimiza watumishi wa afya kufanya kazi kwa weledi kuwahudumia wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Profesa Abel Makubi amesema,  ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere  ulianza mwaka 1975 kwa hatua ya usanifu na ujenzi rasimi  ulianza mwaka 1980.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa hospitali hiyo  umejengwa kwa Awamu nne hadi sasa ambapo ujenzi wa Awamu ya nne umegharimu Shilingi Bilioni 17.1 na ulianza 2019  hadi  Februari 2022, na  kwa sasa Bilioni 16.1 zimelipwa na kufikia asilimia 58 kwa hospitali yote.

 Ameongeza kuwa,  ujenzi huo unatekelezwa na Shirika  la Nyumba la Taifa (NHC) na Mshauri elekezi Chuo Kikuu cha Ardhi  ambapo  hadi sasa  ujenzi  umegharimu Shilingi Bilioni 26.9 na ujenzi wa hospitali yote  ukitarajia kugharimu Shilingi Bilioni 61.1.

Amesema, ujenzi wa awamu ya tano utagharimu Shilingi Bilioni 24 ambapo kwa sasa inatoa huduma ya mama na mtoto pamoja na huduma ya kusafisha figo iliyoanza mwezi Agosti 2020 na wagonjwa wapatao 19,306 wamepatiwa huduma tangu ilipoanza kutoa huduma.

Ameongeza kuwa, kukamililika kwa hospitali hiyo kutawezesha utoaji wa huduma za kibingwa kwa lengo la kuwapunguzia wananchi usumbufu kufuata huduma za kibingwa mbali.  

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Mathew amemuomba, Mheshimiwa Rais kusaidia ufufuaji wa viwanda ambavyo vimekufa vifanye kazi na  visaidie kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Musoma na mkoa kwa ujumla. 

Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini,  Vedastus Mathayo amemuomba Mheshimiwa Rais  Samia kuwezesha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa Stendi  Kuu ya Mabasi ya Musoma ambapo itasaidia kwa kiwango kikubwa kuingiza mapato. 

Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanme Sagini amewaomba wananchi kutii sheria za nchi ili kuondokana na kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali. Huku pia akiwaasa Askari Polisi kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi ili kulinda uaminifu. 

Christina Mdeme ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi amewataka kinamama nchini kujifungulia katika vituo vya afya, Hospitali na Zahanati kwa ajili ya uzazi salama. Huku akiwaonya Wakandarasi wanaokwamisha miradi ya maendeleo kwa kuvaa uzalendo kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news