NA FRESHA KINASA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Miundombinu ya kusafisha na kutibu maji katika Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara unaogharimu Shilingi Bilioni 10.6 ambapo mradi huo utawanufaisha wakazi wa Wilaya ya Bunda na kuchochea shughuli za maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akitoa kitambaa kuweka jiwe la msingi mradi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji pamoja katika viwanja vya Shule ya Msingi Miembeni Wilaya ya Bunda mkoani Mara leo Februari 7, 2022. (Na Mpigapicha Wetu).
Mheshimiwa Rais Samia ameweka jiwe la msingi katika mradi huo leo Februari 7, 2022 ambapo amewataka maafisa wa maji kutobambikia wateja wa maji ankara (bili) kubwa zisizoendana na uhalisia na watumiaji wa maji akiwataka kulipa ankara zao (bili) kwa wakati kuwezesha mradi kujiendesha kwa manufaa endelevu.
Aidha, Rais samia amewataka Wakaguzi wa ndani wa fedha mkoani Mara kusimamia vyema kukagua fedha za miradi na kubaini madudu ya ufujaji wa fedha huku akiwataka viongozi Mkoa wa Mara kuachana na mivutano, uzembe na ufujaji wa mali za umma kwa masilahi ya wananchi.
Pia, Mheshimiwa Rais amekemea miradi kuharibika kabla ya muda wake kufikiwa kutokana na kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.
"Mjenga nchi ni mwenye nchi, nikileta fedha hazifanyi kazi au hazijatumika kwa sababu yoyote ile fedha nazivuta zinarudi,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Mheshimiwa Rais ameongeza kuwa, Mkoa wa Mara miradi kadhaa haifanikiwi na fedha zinaliwa jambo ambalo halina afya katika kujali maisha ya wananchi. Hivyo amewataka viongozi kuwajibika kila mmoja Katika nafasi yake kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa wananchi.
Pia, Rais Samia amewataka Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na makazi ili kufanikisha zoezi hilo liwe na tija kwa maendeleo ya Watanzania.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, amesema kuwa mradi huo utakamilika Aprili 30, 2022 na utazalisha lita Milioni 10 kwa siku kutoka lita milioni 3.7 hapo awali, ambapo mahitaji ya Wananchi wa Bunda ni lita milioni tisa.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema kuwa Rais Samia amewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 708 mkoani humo, ujenzi wa Ofisi za walimu 219, ambapo kila Ofisi ina uwezo wa kuchukua walimu 10, kutoa fedha za kujenga shule mpya 3 ambapo kila shule imepata Milioni 470, pamoja na fedha za ujenzi wa mitaro katika Wilaya ya Bunda.
Hapi ameongeza kuwa, amejipanga kutekeleza maagizo ya Rais Samia ikiwemo kusimamia kikamilifu fedha za miradi zitakazoletwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi. Na akasema tayari mchakato wa kupata wakuu wa Idara wapya katika maeneo yenye utendaji usioendana na kasi ya serikali umefanyika na muda wowote wataanza kazi kusukuma mbele kasi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, Boniphace Getere amemuomba Rais Samia kuwezesha upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) katika Kituo cha afya cha Mugeta pamoja na kusaidia kupata chakula cha bei nafuu kusaidia wananchi ambao mazao yao yamekuwa yakiliwa na tembo na wakati mwingine kuhatarisha usalama wa Wananchi.
Damas Ndumbaro ni Waziri wa Maliasili na Utalii amesema kuwa, wizara hiyo imeendelea kupambana na Wanyama Waharibifu katika Wilaya ya Bunda ikiwemo kutoa elimu kwa vijiji 12 vinavyo pakana na Hifadhi ya Serengeti, kuimarisha doria, kuunda vikundi shirikishi vya ulinzi katika Wilaya ya Bunda vikundi 25, Serengeti vikundi 51, kushirikiana na TAMISEMI ambapo baadhi ya Watumishi watapewa silaha magari kuwezesha mapambano hayo.
Christina Mdeme ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambapo amewataka wakazi wa Bunda kuhakikisha wanalinda miundombinu ya maji kusudi idumu kwa muda mrefu.
Rais Samia amehitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Mara leo.