NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amezindua Kituo cha Pamoja cha Kuhudumia Wawekezaji (One Stop Center) ikiwa ni sehemu ya kuweka mazingira wezeshi na kurahisisha masuala ya uwekezaji mkoani humo.
Kunenge amezindua kituo hicho mjini Kibaha, zoezi ambalo limeshuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mwanasha Tumbo na watendaji wengine.
Akizungumza mara baada ya kuzindua kituo hicho, Kunenge amesema kuwa, kuanzishwa kwa kituo hicho ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kila mkoa kuweka mazingira bora ya uwekezaji.
Amesema,kazi kubwa ya kituo hicho ni kurahisisha kutoa huduma kwa wawekezaji waliopo ndani ya mkoa na hata wale wanaokuja kuwekeza ili kusudi kupanua wigo wa uwekezaji.
"Kituo hiki kitarahisisha kutoa huduma katika mkoa wetu kwa wawekezaji na hilo ni maagizo ya Rais Samia ambapo ameelekeza mikoa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na sisi Pwani tayari tumefanya,"amesema Kunenge.
Kunenge amesema, Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona kila mwekezaji anafanya kazi yake bila usumbufu na katika kudhihirisha hilo ameona bora kukaweka kituo hicho.
Amesema kuwa, kuwepo kwa kituo hicho kitapunguza urasimu unaofanywa na baadhi ya taasisi za Serikali na kwamba kwa sasa mwekezaji akifika katika kituo hicho anapata taarifa zote muhimu.
Amesema kuwa,katika kituo hicho kutakuwa na watu wa Mazingira kwa maana ya NEMC, TARURA, TBS,TRA, DAWASA,Uhamiaji,Zimamoto,Brella,Osha,TANESCO pamoja na sekta nyingine wezeshi ambazo ni msaada kwa wawekezaji.
Amesema, changamoto zote za wawekezaji zitaishia katika kituo hicho na majibu yatapatikana kwa wakati na endapo watashindwa kutatua jambo hilo litasongambele kwa mkuu wa Mkoa kwa ajili ya utatuzi zaidi.
"Uzuri wa kituo hiki kipo karibu na ofisi yangu na nitakuwa nakisimamia muda wote ili kifanye kazi iliyokusudiwa kwa kuwa tunataka Mkoa wa Pwani uzidi kuwa mbele katika masuala ya uwekezaji na hata kibiashara,"amesema.
Aidha, Kunenge amempongeza Rais Samia kwa hatua kubwa aliyofanya ya kuhakikisha wawekezaji wanawekewa mazingira mazuri na kwamba lazima watendaji waunge mkono juhudi hizo.
Awali kabla ya Kunenge kuzindua kituo hicho alitumia fursa ya kukutana na viongozi wa sekta binafsi kutoka TCCIA,Machinga na Wafanyabiashara ili kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili.
Katika kikao hicho viongozi hao walibainisha changamoto zinazowakabili ikiwemo bidhaa zinazozalishwa Pwani kutokuwa na kituo maalumu cha upatikanaji,mwingiliano wa siasa na hata ukosefu wa ushirikiano ambapo Kunenge aliahidi kuzifanyia kazi.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mwanasha Tumbo,amesema kituo hicho kitasaidia kujua idadi ya wawekezaji waliopo mkoani humo sambamba na changamoto zinazowakabili.
Tumbo,amesema kabla ya kuanzisha kituo hicho wawekezaji walikuwa wanakuja na hawafahamiki lakini wanakuja kufahamika pale ambapo wanapatwa na matatizo na kuomba msaada kutoka ofisi za Serikali.
"Utakuta mwekezaji yupo Pwani, lakini Mkuu wa Wilaya hajui,Mkuu wa Mkoa hajui, lakini wanakuja kujulikana pale tu wanapopatwa na matatizo kwa hiyo ninaimani kituo hiki ni suluhisho kwao,"amesema Tumbo.
Hata hivyo, Tumbo amesema kwa sasa kituo hicho kitaanza kufanyakazi siku mbili kwa wiki ikiwa ni Jumanne na Alhamisi huku akiwaomba wawekezaji kutumia kituo hicho kwa ajili ya kuwasaidia kutatua changamoto zao kwa wakati.