NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla amemaliza hali ya taharuki juu ya uvumi wa taarifa zilizodaiwa kuwa eneo la Shule ya Sekondari Kurasini linauzwa kwa mwekezaji ambapo amethibitisha kuwa eneo hilo haliuzwi.
RC Makalla amesema ni kweli kuwa Mwekezaji alituma maombi ya kupatiwa eneo hilo la shule na kuahidi kujenga shule nyingine eneo la Mbagala, lakini Serikali haikuridhia ombi hilo.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kilichojumuisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Temeke, Baraza la Madiwani, Viongozi wa CCM Wilaya, RC Makalla amesema mchakato wa kuuza eneo la shule sio rahisi kwa kuwa ni lazima maombi yaanze ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kisha mkoa upeleke wizarani na wizara iwasilishe ngazi ya juu.
Kutokana na hilo RC Makalla amesema amejiridhisha pasipokuwa na shaka kuwa eneo hilo haliuzwi na halmashauri haina uwezo wa kufanya mauzo ya namna hiyo.
Aidha, RC Makalla amesema kikao hicho pia kimepitia taarifa ya kamati iliyoundwa kupitia dosari zizojitokeza kwenye zoezi la utoaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ya Temeke kwa vikundi vya ujasiriamali ambapo ametangaza kuunda upya kamati ya kufuatilia kwa kina suala hilo ili itoe taarifa sahihi.
Kikao hicho pia kimejadili ajenda ya kufanikisha zoezi la anuani za makazi na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 pamoja na mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Jumapili ya Februari 20,2022.