NA FRESHA KINASA
MJUMBE wa Baraza Kuu la Wanawake Tanzania (UWT) Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly ametoa msaada wa mizinga ya nyuki mitano kwa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Wilaya ya Musoma Vijijini kwa lengo la kuunga mkono juhudi za jumuiya hiyo kuiwezesha kufuga nyuki, baada ya kuibua mradi huo ambao utakuwa na tija kwao.
Pia, Rhobi amekabidhi samani mbalimbali za ofisi ya UWT Mkoa wa Mara zenye thamani ya shilingi milioni 3.3 ikiwemo viti vya kukalia 13 vya ofisi, meza mbili, kabati moja na runinga.
Kwa upande Wake Katibu wa UWT Mkoa wa Mara, Sarah Kairanya wakati akipokea vifaa hivyo mbele ya wajumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara amepongeza hatua ya Rhobi ya kutoa samani kwa ajili ya Ofisi ya UWT Mkoa wa Mara, kwani itawezesha kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa.
Katika kikao cha Baraza la UWT kilichofanyika, Rhobi ameahidi kuendeleza kushirikiana na wanawake wote wa Mkoa wa Mara katika kuunga mkono juhudi za maendeleo kwa kutafuta fursa za maendeleo ambazo zitakuwa na manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Amewahimiza wajumbe wa UWT katika maeneo yao kushiriki kikamilifu mapambano ya ukatili wa kijinsia na amesisitiza mkazo ufanywe na kila mmoja kuhakikisha watoto wa kike wanasoma na kufikia ndoto zao ili waje kuwa msaada katika jamii na Taifa pia.
"Tuendelee kushiriki vyema katika mapambano ya ukatili wa kijinsia, tuhimize watoto wa kike wasome kwa bidii na tuwasaidie kuwaondolea changamoto ambazo ni kikwazo kwao. Mimi naahidi kuendelea kushirikiana na jumuiya kutafuta namna ya kuwainua watoto wa kike kadri Mungu atakavyojalia,"amesema Rhobi.
Aidha, Rhobi ametumia fursa ya kikao cha baraza hilo, kuwaaga wanawake wa jumuiya hiyo kuwa anatarajia kuondoka nchini kuelekea nchini Ufarasa ambapo atakaa huko kwa kipindi cha miezi sita, kutokana na mwaliko wa uongozi wa nchi hiyo kumpa mwaliko wa kwenda kupokea tuzo maalum kutokana na juhudi zake za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia anazozifanya kupitia Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ( HGWT) analoliongoza.
"Wanaweke wa UWT Mara nawasihi sana tuachane na majungu ya kusemana semana sisi kwa sisi. Mfano ukimsema mtu kwa mwingine kusudi tu upate shilingi 50,000. Pesa hiyo itakusaidia Nini? Tutangulizeni mbele upendo, utu, umoja miongoni mwetu na pia tukisemee chama kwa wananchi kwa kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa ufanisi mkubwa,"amesema Wegesa.