NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI
SERIKALI imesema inaendelea kuboresha upatikanaji wa watumishi wa kada za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuendana na upanuzi wa miundombinu ya Afya ya Msingi nchini.
Akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, swali la Mbunge wa Nyangw’ale, Mhe. Nassor Hussein Amar ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi katika vituo vya afya vya Kharumwa na Nyangw’hwale, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Festo Dugange amesema, katika mwaka wa Fedha 2021/22 Serikali iliajiri watumishi 2,726 wa kada mbalimbali za Afya.
Mhe. Dugange amesema, katika ajira hizo za Serikali, Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ilipangiwa watumishi 20 ambapo Kituo cha Afya Kharumwa kilipata watumishi watatu na Kituo cha Afya Nyang’hwale kilipata watumishi wanne.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuajiri na kugawa watumishi kwenye Halmashauri na Vituo vya kutolea huduma za Afya kadiri ya upatikanaji wa vibali vya ajira na fedha ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.