SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA BORA NA WEZESHI KWA KUZINGATIA VIVUTIO VYA KIKODI KWA MIRADI MIKUBWA NA YA KIMKAKATI NCHINI

NA MWANDISHI MAALUM

NAIBU Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaudi Kigahe (Mb.) amesema, Serikali itaendelea kuboresha na kuweka mazingira bora na wezeshi kwa kuzingatia vivutio vya kikodi kwa lengo la kuchochea uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi, kuongeza ajira, kupata fedha za kigeni, biashara za kimataifa na kukuza uchumi.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo wakati wa utoaji wa Taarifa kuhusu utaratibu wa utoaji wa vivutio vya kikodi kwa miradi mikubwa ya kimkakati, mafanikio, changamoto na hatua za kukabaliana nazo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti, Februari 15, 2022 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Akiwa pamoja na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande, Naibu Katibu Mkuu Uwekezaji - Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru, aliwahakikishia wajumbe wa Kamati hiyo kuyafanyia kazi maoni yote waliyotoa katika kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kujenga uchumi endelevu.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Daniel Sillo (Mb.) amesema Wizara inatakiwa kuendelea kuweka vivutio muhimu mbalimbali kwa wawekezaji na kuvifuatilia kama vinatumika ipasavyo na kuonyesha matokeo chanya kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni na mapendekezo yanayolenga kuboresha uwekaji wa vivutio vya kikodi, uwekaji wa kodi zinazofaa, kuimarisha usimamizi na ufanyaji tathmini kwa vivutio vya kikodi vinavyotolewa, kuangalia kwa makini miradi ya kimkakati inayohitaji kodi, kuongeza muda kwa miradi ya kimkakati iliyobainishwa na kuimarisha ulinzi wa wawekezaji wa ndani.

Akitoa taarifa hiyo ya utaratibu wa utoaji wa vivutio vya kikodi kwa wajumbe wa kamati hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uwekezaji wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Aristides Mbwasi alisema katika utaratibu huo, Serikali imefanikiwa kusajiri miradi 42 ya wawekezaji mahiri yenye thamani ya Dola za marekani billion 12.3 na kufanikiwa kutoa vivutio vya kikodi kwa wawekezaji mahiri na wawekezaji mahiri maalum kwa mujibu wa sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news