Serikali yatoa maagizo kwa wakuu wa mikoa kuhusu Sensa

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa yote nchini waendelee kuongeza kasi katika uratibu wa maandalizi ya zoezi la sensa ya watu na makazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Kikao na Wakuu wa Mikoa kwa njia ya mtandao kuhusu Sensa ya Watu na Makazi akiwa Ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Februari 18, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Twende kwa kasi ile ile ili zoezi hili tulimalize kwa ufanisi mkubwa. Watanzania wanatuunga mkono na wanasubiri kwa hamu zoezi hili.” Sensa ya watu na makazi itafanyika Agosti, 2022.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Februari 18, 2022 katika kikao kazi cha viongozi wa mikoa na wilaya kuhusu maendeleo ya maandalizi ya sensa ya watu na makazi.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao, Waziri Mkuu amesema zoezi la uwekaji wa anuani za makazi linatakiwa lisimamiwe vizuri ili likamilike kwa wakati.

“Zoezi hili linatakiwa kutekelezwa kwa operesheni na kwa kipindi maalumu kama ilivyokuwa katika miradi iliyojengwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.”

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kazi nzuri ya kusimamia vizuri shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na utelezaji wa ilani na maelekezo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa kwa upande wa Tanzania Bara, Spika Mstaafu Anna Makinda amesema zoezi hilo wanalitekeleza kwa ushirikiano na viongozi wa ngazi zote kuanzia mkoa hadi vijiji. Amewashukuru viongozi hao na wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa.

Naye, Kamisaa wa Sensa kwa upande wa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza amesema ameridhishwa na kazi kubwa ya sensa ya majaribio iliyofanywa mikoani na amesisitiza juhudi hizo ziendelee ili kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanafikiwa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt, Pindi Chana, Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa.

Wengine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Hassan Chande pamoja na maafisa mbalimbali wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news