NA MWANDISHI MAALUM
WAKANDARASI wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kabingo kwa kiwango cha lami yenye jumla ya urefu wa kilomita 260.6 wametakiwa kukamilisha barabara hiyo kwa kuzingatia ubora kama ilivyosanifiwa ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya njia panda ya Nduta – Kabingo kilomita 62.5 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Kigoma.
Wakandarasi hao ni CHICO anayetekeleza sehemu ya Njia panda ya Nduta – Kabingo KM 62.5, Sinohydro Corporation anayetekeleza sehemu ya Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini kilomita 25.9 na Stecol Corporation anayetekeleza sehemu ya Mvugwe – Njiapanda ya Nduta kilomita 59.35.
Hayo yamesemwa mkoani Kigoma na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipowasili mkoani humo na kukagua maendeleo ya mradi huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, akipitia tarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha sehemu ya Njia panda ya Nduta – Kabingo kilomita 62.5, wakati alipokuwa akikagua mradi huo, mkoani Kigoma.
“Tunategemea barabara hii ikikamilika kujengwa matengenezo yake yaanze baada ya miaka 20, hivyo basi TANROADS kwa niaba ya Serikali hakikisheni mnawasimamia wakandarasi hawa ili tupate barabara yenye viwango vya juu”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Aidha, ameagiza wakandarasi hao kuongeza muda wa kazi na vifaa ili kukamilisha mradi huo mapema zaidi ili kufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri anayesimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami sehemu ya Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini kilomita 25.9, Mhandisi Khatibu Kapombe, wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo, mkoani Kigoma.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Mhandisi Suleiman Bishanga, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa sweta), wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami sehemu ya Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini kilomita 25.9, mkoani Kigoma.
Mhandisi Mshauri anayesimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami sehemu ya Njia panda ya Nduta – Kabingo kilomita 62.5, Mhandisi Felek Amdi, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa sweta), wakati alipokagua hatua ya ujenzi huo, mkoani Kigoma.
“Serikalii itaendelea kulipa fedha za mradi kwa wakati sasa ni jukumu lenu kuongeza muda wa kazi ili kutoongeza gharama za mradi,”amesema Mhandisi Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya ameeleza umuhimu wa barabara hiyo inayounganisha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki kutokea Nyakanazi kwenda Kigoma kupitia makao makuu ya wilaya ya Kibondo ikIunganisha Kasulu hadi Manyovu kwa kiwango cha lami na kutoka Kasulu hadi Burundi kwa barabara ya lami.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Mvugwe – Njiapanda ya Nduta yenye urefu wa kilomita 59.35 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Kigoma. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 29.1, mkoani Kigoma.
Kazi za ujenzi wa barabara sehemu ya Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini yenye urefu wa kilomita 25.9 zikiendelea, mkoani Kigoma. (PICHA NA WUU).
Ameongeza kuwa tayari wakandarasi wapo eneo la kazi kutokea Kigoma ukielekea Tabora kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Malagarasi kilomita 51.1 na Kazilambwa – Chagu kilomita 36 kwa kiwango cha lami
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Eng. Suleiman Bishanga, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa mpaka maendeleo ya ujenzi wa barabara sehemu ya Njia panda ya Nduta – Kabingo kilomita 62.5 imefikia asilimia 20 na unagharimu shilingi Bilioni 95.5 sehemu ya Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini kilomita 25.9 imefikia asilimia 42.1 na unagharimu shilingi Bilioni 31.0 na sehemu ya Mvugwe – Njiapanda ya Nduta kilomita 59.35 imefikia asilimia 29.1.
Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kabingo kwa kiwango cha lami kilomita 260.6 umegawanywa kwa sehemu nne ambazo ni Njia panda ya Kasulu – Manyovu na viunganishi vya barabara za Kasulu mjini KM 68.25, Kanyani – Kidyama – Mvugwe KM 70.5, Mvugwe – Njia panda ya Nduta KM 59.35 na Njia panda ya Nduta – Kabingo KM 62.5.