NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAWAKILISHI pekee wa Afrika Mashariki na Kati klabu ya Simba imeshindwa kutamba ugenini baada ya kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji RSB Berkane.
Ni katika mchezo wa Kundi D Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, mchezo uliopigwa dimba la Stade Municipal de Berkane nchini Morocco.
RSB Berkane walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Adama Ba akitumia vizuri mpira wa adhabu dakika ya 32 akipiga na kwenda wavuni moja kwa moja na kumuacha Aishi Manula akiwa hana la kufanya.
Dakika ya 41 Charki El Bahri aliifungia Berkane bao la pili kwa kichwa akitumia vizuri kona iliyopigwa na Badri hadi mapumziko wenyeji walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko huku Simba wakianza kwa kasi ya kutafuta bao bila mafanikio.
Kwa ushindi huo RSB Berkane wamefikisha alama sita na kupanda hadi kileleni mwa msimamo wa kundi hilo.
Aidha,Simba wanabaki nafasi ya pili wakiwa na alama nne,US Gendarmerie wakishika nafasi ya tatu wakiwa na alama nne huku ASEC Mimosas wakiburuza mkia wakiwa na alama tatu.
Mchezo mwingine wa kundi hilo US Gendarmerie wameutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kuichapa mabao 2-0 ASEC Mimosas.
Kwa mechi hizo timu zote zimemaliza mzunguko wa kwanza na zitaanza kurudiana mwezi ujao.
Tags
Michezo