NA MWANDISHI MAALUM
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) utaanza kutumia mfumo wa Kielektroniki wa malipo ya Ushuru wa Maegesho mkoani Pwani kuanzia tarehe 01 Machi, 2022.
Akifungua semina ya kujengewa uwezo kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amesema mfumo huo unatarajiwa kuanza Machi Mosi mwaka huu na kuomba wananchi mkoani Pwani kupokea mabadiliko hayo na kuhakikisha wanalipa wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka adhabu na faini zisizo za lazima.
Mhe. Kunenge amesema kuwa mfumo huo wa ukusanyaji mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya Moto ( parking fees) na matumizi ya hifadhi za barabara, malipo yote yatafanyika kwa kutumia kumbukumbu namba ya malipo na malipo hayo yatapokelewa Serikalini moja kwa moja.
Ametaja faida ya mfumo huo ni kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya Serikali yatakayosaidia maboresho na maendeleo ya miundombinu ya barabara, utasaidia wateja kufanya maombi na kulipia huduma kwa njia ya mtandao bila kufika ofisi ya TARURA.
"Faida nyingine ni utampa mteja fursa kulipia ushuru wa maegesho kwa saa moja na zaidi, kwa siku, wiki au kwa mwezi.
Ameongeza kuwa utatoza ushuru wa vyombo vya Moto vilivyoegeshwa kwenye maeneo ya maegesho tu na ni mfumo rafiki, rahisi na salama, mtumiaji atatumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa mawakala.
Awali akielezea utekelezaji wa mfumo huo, Mkuu wa Kitengo cha Tehama kutoka TARURA, Ndg. Stanlay Mlula amesema makusanyo hayo yatafanyika kwa maegesho yote yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu na kuomba wananchi na wadau kuhakikisha wanafanya malipo hayo kwa wakati kwa sababu njia inayotumika ni rahisi hasa ya simu za kiganjani ambapo wengi wanakua nayo mahala popote wanapokua.