NA ROTARY HAULE
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umezindua mfumo wa ulipaji ushuru wa maegesho ya vyombo vya moto kwa njia ya kielektroniki ukaoanza kutumika Machi 1, mwaka huu.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge katika kikao cha wadau wa mapato na maduhuli ya Serikali kilichofanyika Mjini Kibaha.
Awali akizungumza kabla ya uzinduzi huo Kunenge amesema kuwa, mfumo huo utarahisisha ulipaji wa ushuru huo bila usumbufu na hivyo kusaidia katika kuongeza mapato.
Kunenge amesema kuwa, awali ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya magari ulikuwa ukilipwa kwa njia ya kawaida ya kukatiwa risiti lakini kwa sasa mfumo umeboreshwa na ushuru huo utalipwa kwa njia ya kielektroniki kupitia simu zao.
Kunenge amesema kuanzisha kwa mfumo huo ni utekelezaji wa mambo makubwa nane yaliyoanzishwa na Rais Samia ikiwemo ukusanyaji wa mapato na kwamba TARURA wameonesha njia.
"Niwapongeze TARURA kwa kuja na mfumo huu wa ulipaji ushuru wa maegesho ya magari kwa njia ya kieletroniki na hii itasaidia kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato na hata uhifadhi wake kuwa wa uhakika,"amesema Kunenge.
Aidha, Kunenge amewataka Wakurugenzi wa halmashauri,wakuu wa taasisi za Serikali zilizopo Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanabuni vyanzo vipya vya mapato ili waweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Kunenge amesema, wakati wanaongeza vyanzo hivyo lazima pia wanaongeza mikakati ya kudhibiti mianya ya upigaji ili kusudi mapato yanayokusanywa yatumike kuleta maendeleo ya sehemu husika.
Meneja mifumo wa TARURA, Stanley Mlula amesema kuwa, ulipaji wa ushuru wa maegesho ya vyombo vya moto sio jambo jipya kwa kuwa ulikuwa siku nyingi isipokuwa TARURA wameboresha namna ya ulipaji wake.
Mlula amesema, tayari mfumo huo umeanza katika mikoa mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Singida,Iringa,Mwanza, Morogoro,Dar es Salaam na sasa kuingia Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa,kwa upande wa Mkoa wa Pwani mfumo huo utaanza kutumika Machi 1, mwaka huu na itahusisha eneo lote la hifadhi ya barabara huku vyombo vitakavyotakiwa kulipa ni pikipiki yenye magurudumu mawili,bajaji na gari.
Mlula ameongeza kuwa, mtu anaweza kulipia maegesho kupitia simu yake ya mkononi kwa kupiga *152*00# na baadae atakwenda namba mbili kwenye neno TARURA na atachagua namba tatu ya lipia maegesho.
Amesema,baadae ataingiza namba nne itakayomtaka kuingiza namba ya chombo na kisha kupokea ujumbe utakaompa mwongozo wa kukamilisha muamala wa ulipaji ushuru huo.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji amemshukuru Mkuu wa Mkoa huo kwa kufanya uzinduzi huo na kwamba matarajio ya mfumo huo ni kuongeza mapato ya Serikali yanayotokana na TARURA.
Runji amesema kuwa, viwango vya kulipa ushuru huo kwa siku ndani ya Mkoa wa Pwani ni kuanzia sh.200 kwa pikipiki,300 bajaji na gari 500 na kwa mwezi pikipiki sh. 4,000,bajaji sh.6,000 huku gari sh.10,000.
Hata hivyo,Runji amesema kuwa, mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 14 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa ushuru na maegesho pamoja na faini ya sh.10,000.