NA MWANDISHI MAALUM-TARURA
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kutoa elimu ya mfumo wa maegesho Kidigitali kwa wananchi mkoani Morogoro kupitia Redio Abood FM pamoja na Abood Tv zilizopo mkoani humo.
Akizungumza na wananchi kupitia vyombo hivyo, Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mboka Nkwera amewafahamisha wananchi wa Mkoa huo kuwa kuanzia tarehe 1 Machi, 2022 mfumo mpya wa kulipia maegesho kwa njia ya kielektroniki utaanza kutumika.
Mhandisi Mboka amefafanua kuwa mfumo huo ni rahisi, rafiki na salama na utadhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali kwani umeunganishwa na mfumo wa GePG ambapo malipo yanafanyika kwa kutumia “Control number”.
Pia ameongeza kuwa mtumiaji wa maegesho atalipia maegesho ndani ya Siku 14 baada ya kutumia maegesho huku mwenye gari atalipa Shilingi 300 kwa saa na Shilingi 1,000 kwa Siku, Pikipiki yenye magurudumu mawili (Bodaboda) Shilingi 300 kwa Siku na Pikipiki yenye magurudumu matatu (Bajaji) Shilingi 500 kwa Siku.
Naye Mtaalamu wa Mifumo, Bw. Shadrack Mahenge ameelezea namna mfumo unavyofanya kazi kwamba mtumiaji wa maegesho anapotumia maegesho atascaniwa chombo na kupatiwa Ankara/Bili yenye kumbukumbu namba ambayo atatumia kulipia maegesho kwa kutumia simu ya mkononi kwa kupiga *152*00# na kufuata maelekezo, kupitia App ya TeRMIS na GePG zinazopatikana Play Store na App Store, kupitia Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala.
Kwa upande wake Mhasibu wa Mapato, Bw. Oswald Mobily ameeleza kuwa mtumiaji wa maegesho anaweza kujisajili ili aweze kupata ujumbe mfupi wa deni pale anapotumia maegesho kwa kupiga *152*00# kisha kufuata maelekezo ambapo namba hiyo inatumika kusajili, kufanya malipo na kuangalia deni.
Vile vile ukishakuwa na kumbukumbu namba unaweza kufanya malipo kupitia mtandao wowote wa simu kwa kuchagua malipo ya Serikali.
TARURA inaendelea kutoa elimu ya maegesho kidigitali mkoani Morogoro ili wananchi waweze kuufahamu mfumo na kuweza kuutumia ambapo mfumo unatarajia kuanza kutumika Machi 1, 2022.