TEA, BRAC Maendeleo Tanzania wasaini makubaliano kuongeza ufanisi Sekta ya Elimu

NA ELIAFILE SOLLA-TEA

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) na Shirika lisilo la Kiserikali la BRAC-Maendeleo Tanzania wamesaini makubaliano maalum ambayo yamelenga kuongeza ufanisi katika Sekta ya Elimu jijini Dar es Salaam.

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo imefanyika leo Februari 10, 2022 makao makuu ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) yaliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati Geuzye (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania, Bi. Susan Bipa wakisaini makubaliano maalum kwa ajili ya kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu katika Jiji la Dar es Salaam. (Picha na TEA).

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bi. Bahati Geuzye amelipongeza Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini. 

"TEA tunaona fahari kushirikiana na BRAC - Maendeleo Tanzania katika jukumu hili kwa manufaa ya sekta ya elimu na kuchangia maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla,"amesema Bi.Geuzye.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA amesema kuwa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. 

Amesema, TEA ilianzishwa mwaka 2001 kwa Sheria ya Bunge Na. 8 kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao pia ulianzishwa mwaka 2001 ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa nchini. 
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati Geuzye (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania, Bi. Susan Bipa wakionesha wajumbe wa Menejimenti ya TEA (hawapo pichani) makubaliano maalum waliosaini kwa ajili ya kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu katika jiji la Dar es Salaam. (Picha na TEA).

"Kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, TEA inafadhili ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, mabweni, mabwalo na majiko yake, maabara na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara na ngazi ya Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar. 

"Kupitia Mfuko wa Elimu pia ukarabati mkubwa unafanyika katika taasisi za elimu zikiwemo shule za Sekondari ambapo TEA imeshiriki katika kukarabati shule kongwe 17 za sekondari kati ya 89 zilizopo katika mpango huo wa ukarabati. Hivi karibuni, TEA imeshiriki kukarabati shule nne za msingi katika Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi iliyochangiwa na uamuzi wa Serikali kuhamia rasmi katika jiji hilo,"amesema Bi. Bahati Geuzye.

Amesema, makubaliano ya ushirikiano maalum na Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania ambalo ni mdau muhimu wa maendeleo katika Sekta ya Elimu nchini yana mchango mkubwa katika kuinua viwango na ubora wa elimu nchini.

"TEA inasaini makubaliano haya ya ushirikiano baina yake na BRAC Maendeleo Tanzania kwa vile yatachangia kusukuma mbele jitihada za nchi yetu katika kufikia lengo namba Nne la Maendeleo Endelevu ya Millenia linalohimiza elimu bora, yenye usawa na kutoa fursa kwa wote kujiendeleza. 

"Aidha makubaliano haya yanaenda sanjari na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2021/22- 2025/26 ambao pamoja na mambo mengine unahimiza kukuza na kuwezesha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufundisha na kujifunza katika ngazi zote za elimu nchini. Mpango huo pia unahimiza ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu katika shule za Msingi, Sekondari na katika ngazi ya vyuo,"amesema Mkurugenzi Mkuu wa TEA.

Pia amebainisha kuwa, kupitia makubaliano haya tunayosaini leo, katika mwaka wa kwanza BRAC - Maendeleo Tanzania, imepanga kutoa Kompyuta 120 ambazo zinajumuisha Kompyuta Mpakato 60 na Vishikwambi (Tablets) 60 zikiwa na thamani ya Shilingi Milioni 132.6. 

Amesema, kompyuta hizo zitapelekwa katika shule tatu za Sekondari katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambazo ni Miburani, Wailes na Karibuni. 

"Shule nufaika zitakuwa na vyumba maalum vya kompyuta (Computer Lab) vitakavyotoa fursa ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo elimu ya Kompyuta. Msaada huu utanufaisha wanafunzi 600 na walimu 26 katika shule hizo

"Tunawapongeza sana BRAC Maendeleo Tanzania ikizingatiwa kwamba tunaishi katika zama za Sayansi na Teknolojia ambapo shughuli nyingi zinafanyika ki-dijitali ikiwa ni pamoja na masomo. Hivyo Kompyuta zilizotolewa katika shule hizi za jijini Dar es Salaam zitatoa fursa kwa wanafunzi kupata maarifa hata kwa njia ya mtandao.

"Nichukue fursa hii kusihi shule zilizonufaika na msaada huu wa kompyuta kuzitumia na kuzitunza vizuri ili zidumu na kunufaisha kundi kubwa la wanafunzi. Kama tunavyofahamu vifaa hivi vinahitaji utunzaji maalum ikiwa ni pamoja na kuwa na vyumba vinavyofaa, hivyo shule nufaika zijiandae vyema kwa hili.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye (wa pili kushoto) akipokea moja ya Kishikwambi (Tablet) zitakazopelekwa kwenye baadhi ya shule za jijini Dar es Salaam kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania Bi. Susan Bipa (kushoto). Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa miradi kutoka TEA Bi. Anna Makundi pamoja na Mkurugenzi wa huduma za Taasisi TEA, Dkt. Erasmus Kipesha.(Picha na TEA). 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania, Bi. Susan Bipa ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuanzia Serikali Kuu hadi ngazi za mitaa kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakiupata katika utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.

Amesema, hapa nchini BRAC inashirikiana na shirika dada la BRAC Tanzania Finance Limited kutoa huduma ndogo za kifedha kwa wajasiriamali wadogo na hasa akina mama.

"Toka mwaka 2020, tumekuwa tunatekeleza mradi huu wa Skills for their Future ukiwa ndani ya mpango wetu wa Uwezeshaji Vijana (Youth Empowerment). Mradi huu unafanyika chini ya ufadhili wa Shirika la TheirWorld lenye makao makuu nchini Uingereza,"amesema Mkurugenzi wa Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania Bi. Susan Bipa.

"Lengo kuu la mradi ni kushughulikia changamoto zinazozuia wasichana na wanawake wadogo kuweza kupata huduma za TEHAMA na kuzitumia kwa ufanisi ili kuboresha ujuzi katika ujasiriamali na kuongeza uwezo wa kujiajiri,"amesema.

Pia amefafanua kuwa, BRAC Maendeleo Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa ufadhili wa Shirika la Their World wanatarajia kufanya Mradi wa Ujuzi Endelevu kwa Maisha ya Baadae.

Amesema, kupitia mradi huo utasaidia kuongeza ushiriki wa wasichana katika TEHAMA ili kuongeza fursa zaidi za ajira kwa wasichana katika sekta ya teknolojia.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati Geuzye (wa pili kushoto) akipokea moja ya kompyuta mpakato zitakazopelekwa kwenye baadhi ya shule za jijini Dar es Salaam kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la BRAC - Maendeleo Tanzania Bi. Susan Bipa (kushoto). Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa miradi kutoka TEA Bi. Anna Makundi pamoja na Mkurugenzi wa huduma za Taasisi TEA, Dkt. Erasmus Kipesha. (Picha na TEA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news