NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa Kimbunga Batsirai katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
TMA imesema kimbunga hicho tangu kilipojitokeza katika Bahari ya Hindi, Januari 27, 2022 kwa sasa kimesogea katika maeneo ya kisiwa cha Madagascar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 4,2022 na mamlaka hiyo imesema uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kutokuwepo kwa uwezekano wa Kimbunga hicho cha Batsirai kufika katika Pwani ya Tanzania.
Imeeleza kuwa, uwepo wa kimbunga hicho baharini unatarajiwa kuathiri mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha ongezeko la mvua, vipindi vya upepo mkali unaofika na kuzidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa baharini yanayozidi mita mbili hasa kwa maeneo ya Ukanda wa Pwani.
Aidha,taarifa hiyo imetaja maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa kutokana na uwepo wa kimbunga hicho baharini kati Februari 4 hadi 8 mwaka huu ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi , Ruvuma, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa.
Hata hivyo mvua za Msimu zinaendelea katika maeneo mengine yanayopata mvua hizo.
Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Pia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho.
Tags
Habari