UWT yagusa maisha ya wasichana wanaopewa hifadhi Kituo cha Nyumba Salama

NA FRESHA KINASA

JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) chini ya Mwenyekiti wake, Gaudencia Kabaka imetembelea Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama kinachotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni chini ya Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo mchele kilo 100, maharage kilo 100, sabuni boksi tisa pamoja na mafuta ya kupaka boksi mbili. 
Misaada hiyo imetolewa leo Februari 3, 2022 kituoni hapo katika kuadhimisha miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi na kuunga mkono kazi nzuri zinazofanywa na shirika hilo chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekuwa wakishiriki kuvipinga. 
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudencia Kabaka amesema kuwa, jumuiya hiyo ipo bega kwa bega na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo haitarudi nyuma hata kidogo kutetea na kupigania haki na usawa kwa kushirikiana na Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye yuko mstari wa mbele kuhakikisha vitendo vya ukatili vinakwisha hapa nchini sambamba na kutambua mchango mkubwa wa maendeleo unaofanywa na wanawake katika sekta mbalimbali.
Kabaka ameongeza kuwa, anashukuru kuona Kituo hicho cha Nyumba Salama chini ya Shirika la (HGWT) kinatoa Hifadhi kwa Wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili na kupewa hifadhi na kuendelezwa kielimu ili wafikie ndoto zao ambapo ameishauri jamii pia kuachana na mila zisizofaa ambazo zinafifisha juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wa kike wanasoma na kufikia malengo yao ikiwemo ili wachochee maendeleo katika jamii na Taifa pia. 
Kwa upande wake Afisa Mwelimishaji Jamii madhara ya Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck akizungumza na DIRAMAKINI BLOG, ameishukuru UWT kwa kutembelea Kituo hicho na kutoa misaada hiyo ambapo amesema itawasaidia wasichana wanaoishi kituoni hapo. 

Ameongeza kuwa, shirika hilo litaendelea na utoaji wa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali wakiwemo Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia na makundi mbalimbali katika jamii kwa kuendesha makongamano na mikutano ya hadhara sambamba na kutoa elimu shuleni kwa wanafunzi ili wawe mabalozi wa kupinga ukatili na kutoa elimu katika maeneo yao.
"Tunaishukuru sana UWT Taifa kuja kituoni hapa Nyumba Salama na kutoa misaada hii, hakika huu ni upendo wa kipekee waliouonesha kwa wasichana waliopo kituoni hapa. Wametambua kazi tunayoifanya hakika Mungu aweze kuwabariki Sana walipotoa akazidishe baraka na neema nyingi kwao,"amesema Goodluck. 
Aidha, jumuiya hiyo imefanya maadhimisho yake kitaifa katika Wilaya ya Butiama ya miaka 45 ya CCM sambamba na kutoa misaada mbalimbali katika baadhi ya shule za sekondari ikiwemo taulo za kike, kushiriki katika shughuli za kufuatilia juu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025, kupanda miti, na kutoa mashine ya kusaidia watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama, kuhamasishana kujitokeza katika zoezi la Sensa pamoja na kuhimizana viongozi wa UWT kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO-19 katika maeneo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news