Waandishi, wafanyakazi wampa Bilionea Rostam Aziz siku 14 tu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayomilikiwa na bilionea na mfanyabiashara maarufu wa Kimataifa, Rostam Aziz chini ya Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Hussein Bashe imepewa saa 336 sawa na siku 14 kulipa mafao yao. 

Hayo yameelezwa kupitia tamko la pamoja lililotolewa leo Februari 3, 2022 na wafanyakazi wa New Habari (2006) Ltd inayomiliki magazeti ya Mtanzania,The African, Rai, Dimba na Bingwa wanaodai mafao yao.

"Ndugu wanahabari, baada ya kuchoshwa na hali hii, sisi wafanyakazi tumeamua yafuatayo; tunampa siku 14 kuanzia leo mwekezaji na mmiliki wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Bilionea Rostam Aziz awe amepeleka fedha zetu
za mafao katika mifuko ya hifadhi husika.

"Endapo asipotekeleza takwa hilo tutafanya maandamano ya amani yasiyokuwa na ukomo nyumbani kwa Rostam Aziz, ofisini kwa Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe na Ofisi za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na PSSSF) hata kama hatua hiyo itagharimu maisha yetu. Tupo tayari,"wamedai.

Wafanyakazi hao wamesema, wamewaita wanahabari leo kwa lengo moja kwamba wasaidie kufikisha taarifa zao," Ni kwa Serikali yetu Tukufu inayoongozwa na Mama yetu mpendwa, Rais Samia Suluhu Hassan tukieleza juu ya madhila yaliyotupata na yanayoendelea kutupata baada ya aliyekuwa mwajiri wetu, Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayomilikiwa na bilionea na mfanyabiashara maarufu wa Kimataifa, Rostam Aziz chini ya Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Hussein Bashe kutopeleka fedha za mafao.

"Bilionea huyo ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Caspian Ltd inayomiliki asilimia 31.5 ya hisa katika Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamonds Ltd (WDL) mkoani Shinyanga hivi karibuni alinukuliwa na baadhi ya vyombo
vya habari nchini akiweka wazi kuwa pia ana mahusiano ya kibishaara na makampuni mengine mbalimbali ya uchimbaji madini kama, Petra, De Beers, Barrick na AngloGold Ashanti.

"Bilionea huyo kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe walituondoa kazini Mei mwaka 2019 bila kutulipa stahiki za mafao yetu kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) na PSSSF kwa mujibu
wa sheria.

"Ndugu wanahabari, Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, iliyokuwa chini ya Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) Hussein Bashe ambaye sasa ni Waziri wa Kilimo ilituondoa kazini kwa lazima wafanyakazi wake wote bila kutangaza kwa umma sababu za kufanya hivyo kama sheria inavyotaka.

"Pamoja na hatua hiyo hawakutulipa mafao ya NSSF na PPF ambayo sasa inajulikana kama PSSSF kama walivyokuwa wameahidi wakati wanatuondoa kazini.

"Ndugu wanahabari, Ukandamizaji huu wa haki zetu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi ni kinyume kabisa na msimamo wa Serikali ya Rais wetu mpendwa,Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua kuwa mstari wa mbele katika kutetea na kulinda haki za watu wote hususani wananchi wanyonge.

"Kwa mfano hivi karibuni Serikali ilitoa ofa maalum ya msamaha wa asilimia 100 kwa waajiri wa sekta binafsi wanaodaiwa na wenye malimbikizo makubwa ya madeni ya mafao ya wafanyakazi kulipa madeni yao bila riba yoyote. Msamaha huo ulianza Oktoba Mosi 2021 hadi Januari 31,2022 na kuwaondolea tozo zote zitokanazo na ucheleweshwaji wa michango husika kwa kiwango cha asilimia 100.

"Hata hivyo mpaka muda huu tunapozungumza nanyi, mwajiri wetu bado hajafanya chochote licha ya kwamba aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe ni Waziri katika Serikali hii.

"Aidha, mfano mwingine mzuri wa Serikali yetu sikivu katika kutetea wanyonge,ambao kila mtu anaujua ni agizo la siku saba kwa waajiri na wamiliki wote wa vyombo vya habari nchini wenye madeni ya waandishi wa habari wakiwemo waliofariki dunia katika ajali ya gari wilayani Busega mkoani Simiyu hivi karibuni kulipwa stahiki zao yakiwamo malimbikizo ya mishahara na mafao yao.

"Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye kwa niaba ya Serikali alitoa kauli hiyo wakati wa utoaji wa heshima za mwisho na kuaga miili ya waandishi hao watano pamoja na dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.Ngoja tunukuu;

“......Nimepewa salamu hapa kuwa miongoni mwa waliolala kwenye majeneza haya mbele yangu hawajalipwa stahiki zao; natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa kulipa stahiki zote za marehemu na kutoa taarifa ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza,” aliagiza Nape.

"Kwa kukazia hilo, Serikali yake iliwataka wamiliki wa vyombo vya habari wanaodaiwa kutambua kwamba Serikali ndiyo imeshikilia leseni zao. Hilo ni Onyo tosha!.

"Kwa kauli na msimamo huu wa serikali, tunaamini kilio chetu hiki kitapatiwa ufumbuzi wa haraka kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Hivyo basi tunawaomba pia washirika wake mbalimbali wa kibiashara wa nje na ndani
yakiwemo makampuni ya Kimataifa anayofanya nayo biashara yakiwemo Kampuni za uchimbaji madini zinazoheshimika sana duniani wamshauri Bilionea Rostam Aziz kufuata sheria za nchi na haki za binadamu kwa kulipa mafao halali ya wafanyakazi.

"Ndugu wanahabari,Wakati wote wa ajira, mwajiri wetu Kampuni ya New Habari (2006) Ltd chini ya Hussein Bashe akiwa Mbunge na sasa Waziri wa Kilimo alishindwa kabisa kuwasilisha kwenye mifuko michango yetu yote ya mafao ya wafanyakazi ambayo alikuwa akitukata kupitia mishahara yetu ya kila mwezi pamoja na michango ya
mwajiri kwa mujibu wa sheria kwa zaidi ya miaka 10.

"Ndugu wanahabari: Licha ya sisi wafanyakazi kuhoji mwenendo huo, siku zotemwajiri alituaminisha kwamba anapeleka makato yetu katika mifuko husika. Hata hivyo tunashangaa watendaji wa mifuko hiyo kutochukua hatua yoyote kwa mwajiri kwa zaidi ya miaka 10 tofauti na sheria iliyounda mifuko hiyo inavyoelekeza.

"Ndugu wanahabari, mafao tunayoidai Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni zaidi ya Sh Bil 3.4 kwa wafanyakazi zaidi ya 200, miongoni mwetu wengine wakiwa wamekwishatangulia mbele ya haki huku wakiacha familia na watoto wao wakizidi kuteseka.

"Baadhi ya wenzetu waliotangulia mbele ya haki bila kupata mafao yao ni pamoja na aliyekuwa Mhariri wa habari Kanda ya Kaskazini, Eliya Mbonea, Mhariri wa Maudhui ya habari wa Kampuni, Mwalimu Chrysostom Rweyemamu, Mhariri wa habari wa gazeti la Rai, Innocent Mnyuku, Mhariri wa Makala wa gazeti la RAI, Mayage S. Mayage, Mhariri wa magazeti ya Michezo, Asha Muhaji, Afisa Utawala Msaidizi, Benjamin Mhina pamoja na Katibu muhtasi Mama Maidan Jumanne.

"Ndugu wanahabari, sasa ni mwaka wa tatu tumeendelea kupigania haki ya mafao yetu bila mafanikio licha ya kupeleka malalamiko yetu sehemu mbalimbali zinazohusika ikiwamo NSSF pamoja na iliyokuwa PPF sasa PSSSF, lakini hakuna hatua zozote za wazi zinazoonekana kuchukuliwa kuhakikisha sisi wahanga tunalipwa mafao yetu ambayo ni haki yetu.

"Ndugu wanahabari, hapa tulipofika tumechoka na tunasema wazi kwamba hatuna imani na watendaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwakuwa wameshindwa kuwajibika kwa kuwabana aliyekuwa mwajiri wetu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe na Bilionea Rostam Aziz.
"Kwa msingi huo, ndiyo maana tunadhani kuna mchezo mchafu unaendelea kati ya mifuko na mwajiri wetu. Tunafahamu kuwa PPF waliwahi kuishtaki Kampuni ya New Habari na kushinda kesi mwaka 2012, katika kukazia hukumu mahakama iliamuru kukamatwa mali za New Habari (2006) Ltd kupitia Kampuni ya udalali ya Tambaza. 

"Hata hivyo zoezi hilo halijawahi kutekelezwa mpaka PPF inabadilishwa kuwa PSSSF. Ndugu waandishi wa habari, baada ya wafanyakazi kuondolewa kazini wapo waliokwenda kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kufuatilia fao la kutokuwa na ajira kwa mujibu wa sheria, lakini walishindwa kupata haki hiyo kwakuwa mwajiri hakuwahi kuwasilisha makato yoyote licha ya kuwakata kwenye mishahara yao kila mwezi,"wameongeza wafanyakazi hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news