NA HUGHES DUGILO
WADAU wanaoshiriki mafunzo ya watoa huduma katika mnyororo wa Sekta ya Utalii yanayoendelea Katika Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wamekiomba Chuo cha Taifa cha Utalii kufungua tawi lake katika Ukanda wa Kusini ili kutoa fursa kwa vijana wa maeneo hayo kupata elimu na ujuzi katika fani mbalimbali ikiwemo ya utalii.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi Sedoyeka akizungumza na wadau wanaoshiriki mafunzo ya watoa huduma katika mnyororo wa Sekta ya Utalii yanaofanyika kwa siku tano Songea mkoani Ruvuma.Dkt. Sedoyeka amewatembelea wadau hao kujionea shughuli za ufundishaji zinavyoendela na kupata maoni yao kuhusu mafunzo hayo.
Wadau hao wametoa maombi hayo kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi Sedoyeka alipowatembelea na kuzungumza nao kwa lengo la kupata maoni yao kuhusu mafunzo hayo.
Dkt. Sedoyeka amewaeleza wadau hao nia njema ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano dhidi ya UVIKO 19 na kwamba mafunzo hayo yanalenga kusaidia Sekta hiyo kwa kuhakikisha kila mdau anapata uelewa sahihi wa namna ya kukabiliana na janga hilo.
"Ndugu zangu nimekuja kuwatembelea kuona vile mnavyopata mafunzo haya, lakini pia kupata maoni yenu kuhusiana na mafunzo haya," amesema Dkt. Sedoyeka.
Mzee Richard Charles mshiriki wa mafunzo hayo akiwasilisha maoni yake kuhusu mafunzo hayo.
Aidha amesema kuwa amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wadau hao waliofika kushiriki mafunzo hayo kutoka Katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma, na kwamba ana imani kubwa mafunzo hayo yatawawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni za kujikinga na UVIKO 19.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Kwa wakati tofauti wametoa maoni yao kwa Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mshiriki wa Mafunzo Tulahigwa Kaduma akiwasilisha maoni yake kwa Chuo Cha Taifa cha Utalii.
Tulihigwa Kaduma ni mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Songea amekipongeza Chuo hicho kupeleka mafunzo Mkoani humo huku akiomba uongozi wa Chuo hicho kufungua Tawi lake Katika mikoa ya kusini ili kutoa fursa kwa vijana wao kupata Elimu ya Mambo mbalimbali katika Sekta hiyo.
"Niombe pia uongozi wa Chuo mfungue Tawi lenu huku kusini kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmewasaidia vijana wetu kupata Elimu Katika fani hii,"amesema.
Anthony Masebe Mshiriki wa Mafunzo hayo kutoka Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori Tanzania (TAWA) akitoa ufafanuzi kuhusu vibali vya kuanzisha mabucha ya wanyamapori. (PICHA NA HUGHES DUGILO).
Na kuongeza kuwa "Lipo jambo lingine tulikuwa tunaomba mtusaidie kupata vibali vya kuwezesha uwepo wa mabucha ya wanyamapori ili wadau waliopo kwenye Sekta hiyo waweze kupata kipato" aliongeza Tulahigwa, huku Dkt. Sedoyeka akimkaribisha Afisa Mhifadhi wa Mkoa wa Ruvuma kutoka Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori Tanzania (TAWA) Anthony Masebe kulitolea ufafanuzi.
Katika hatua nyingine akizungumza kwenye mahojiano maalum Mratibu wa Mafunzo hayo Mkoa wa Ruvuma Elina Makanja amesema kuwa mafunzo hayo yanaendelea vizuri katika Mkoa huo na kwamba kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wadau hao ambapo jumla ya washiriki 124 kutoka katika Wilaya zote za Mkoa huo wanashiki Mafunzo hayo.
Msimamizi wa mafunzo katika Mkoa wa Ruvuma na Mkufunzi Mwandamizi wa masomo ya Lugha na ujuzi wa Mawasiliano wa Chuo cha Taifa cha Utalii Elina Makanja akifundisha somo la masiliano ya kitaalamu Katika utoaji wa huduma za utalii na Ukarimu kwa wadau wa sekta ya utalii Mkoani Ruvuma.
"Kwakweli mafunzo haya yanakwenda vizuri sana tumepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wetu na maudhurio ni mazuri sana, washiriki wanauliza maswali na kunakuwa na majadiliano ya pamoja katika kila mada kwakweli tunakwenda vizuri sana,"amesema Elina.
Mafunzo hayo ya siku tano yanaendelea Mkoani Ruvuma ikiwa ni muendelezo, ambapo pia yanatolewa katika mikoa nane ikijumuisha Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Mara na Mwanza. Ambapo mpaka sasa mafunzo hayo yamekamilika katika mikoa ya Lindi na Mtwara, na sasa yanaendelea katika mkoa wa Ruvuma na Njombe.