NA GODFREY NNKO
WAKULIMA wadogo kwa wakubwa nchini wameshauriwa kutumia fursa za mikopo ya kilimo inayotolewa na benki nchini ili kupanua shughuli zao za kilimo na kulima kisasa kwa matokeo makubwa zaidi.
Meneja Uchumi Tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mbeya, Dkt. Nicholaus Kessy ameyasema hayo leo Februari 14, 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusu Utayarishaji na Utekelezaji wa Sera ya Fedha katika siku ya kwanza ya semina ya siku tano iliyoandaliwa na Benki Kuu kwa waandishi wa habari za biashara, uchumi na fedha katika Ukumbi wa Benki Kuu Tawi la Mbeya.
Dkt.Kessy amesema, shughuli za kilimo nchini zina mchango mkubwa katika Pato la Taifa, na ni njia ya haraka kuliwezesha Taifa na jamii kusonga mbele kiuchumi.
"Kilimo nchini kinashirikisha wananchi wengi, hivyo wakipatiwa fedha na mazingira rafiki ya kutekeleza shughuli zao za kilimo, mafanikio yatakuwa makubwa sana. Ndiyo maana Benki Kuu iliona kuna umuhimu wa kuzielekeza benki kutoa mikopo nafuu katika sekta ya kilimo.
"Na ile dhana kwamba walengwa wa mikopo hiyo ni wakulima wakubwa tu, sio sahihi. Mikopo ya kilimo ni kwa wakulima wote, hata mkulima mdogo akitimiza matakwa ya benki atapatiwa mkopo kwa ajili ya shughuli zake za kilimo,"amesema Dkt. Kessy.
Pia amefafanua kuwa, dhamira ya mikopo hiyo ni kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kufanya tafiti, utifuaji, mbegu, mbolea,upandaji, mavuno, uchakataji, uhifadhi na hatimaye kwenda sokoni iwe ndani au nje. Amesema, shughuli za kilimo ni pana kwani pia zinajumuisha ufugaji ambao unafanyika hapa nchini.
Awali Dkt.Kessy akisoma hotuba kwa niaba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Dkt. Bernard Kibesse amesema, Tanzania ina fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo shughuli za kilimo ambazo wanahabari wanapaswa kuziibua na kuwashirikisha wananchi ili wajue pa kuanzia kwa ajili ya uzalishaji.
"Mfano mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo hazijatumika ipasavyo ili kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi yetu. Fursa hizo ni pamoja na ardhi nzuri ifaayo kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hali ya hewa nzuri, pamoja na vivutio vingi vya utalii.
"Waandishi wa habari pamoja na vyombo vyenu mna nafasi ya kuziibua fursa hizo kwa kuzitangaza ili kuwavuta wawekezaji na watalii kufika katika mikoa hii na kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
"Kwa mfano, Nyanda za Juu Kusini zina vivutio vingi vya utalii kama Mbuga za Taifa za Kitulo, Ruaha na Katavi, ambazo hazipati wageni wengi wa ndani na nje ya nchi pengine kwa sababu hazitangazwi sana,"amesema Dkt.Kibesse.
Amefafanua kuwa, waandishi wa habari wakidhamiria kubadilisha hali hiyo wanaweza na kuifanya kanda hiyo iwe maarufu kama ilivyo Kanda ya Kaskazini kwa masuala ya utalii.
Pia amesema hivi karibuni limeibuka zao la parachichi, ambalo linahitajika sana siyo hapa nchini tu, bali pia nje ya nchi.
"Pamoja na zao hilo, hali ya hewa katika Nyanda za Juu Kusini inaruhusu kilimo cha mbogamboga na matunda kwa soko la ndani na la nje. Kwa sasa, nyanda hii imejaliwa kuwa na uwanja wa ndege mkubwa ambao unaweza kutumika kwa ajili ya kusafirishia mazao hayo kwenda nje ya mikoa hii na hivyo kuwaongezea wananchi kipato.
"Natoa wito kwa waandishi wa habari kutumia taaluma yenu kuhimiza wananchi kujishughulisha na kilimo cha mazao hayo na mengine kwa wingi ili kunufaika na fursa za masoko zilizopo. Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnachangia kuongeza uzalishaji hapa nchini, kuwafanya wananchi wajiongezee kipato kutokana na mauzo ya mazao hayo na kuliwezesha taifa kupata fedha za kigeni kwa mazao yatakayokuwa yanauzwa nje ya nchi,"amefafanua. Dkt. Kessy kwa niaba ya Dkt.Kibesse.