NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)
ARDHI nzuri tunayo, ya kuzalisha mazao,
Mazao mengi tunayo, ya chakula huku kwao,
Na ya biashara nayo, Nyanda Kusini ni kwao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji zaidi.
Huyu Naibu Gavana, ni Benki Kuu yao,
Hili jambo ameona, ya kwamba ni kazi yao,
Wanahabari kuona, lataka juhudi zao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji zaidi.
Upande uwekezaji, utalii na mazao,
Ni hamasa si kipaji, kuwahamasisha wao,
Wafike wawekezaji, tupate mitaji yao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji Zaidi.
Uchumi wa nchi yetu, ni kazi yetu na yao,
Tukibaki peke yetu, hatutawafikia wao,
Wanapowekeza kwetu, tutakuwa kama wao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji Zaidi.
Vivutio utalii, ni vingi kuliko kwao,
Tuwalete nchi hii, wasafishe macho yao,
Sisi tusibaki zii, tuzivune pesa zao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji zaidi
Mbuga Ruaha ya kwetu, Wanyama si kama kwao,
Katavi kuzuri kwetu, Wanyama kwetu mazao,
Daraja la Mungu letu, na wala haliko kwao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji zaidi.
Uzidi uwekezaji, hapa kwetu sio kwao,
Na hata uzalishaji, faida yetu si yao,
Iongezeke mitaji, tufikie levo yao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji zaidi.
Serikali yawezesha, mazingira kama kwao,
Mlolongo yafupisha, walete mitaji yao,
Nanyi mkihamasisha, tutawavutia hao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji Zaidi.
Kaskazini twaona, kwa maendeleo yao,
Ngorongoro twaiona, wengi waja toka kwao,
Na sisi vema kuona, wageni kutoka kwao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji Zaidi.
Kalamu runinga bora, kuwaleta toka kwao,
Tutangaze zetu sera, ziwavutiao wao,
Ni faida si hasara, tutapata pesa zao,
Waandishi hamasisha, uwekezaji zaidi.
Imeandaliwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)