Waziri Bashungwa amesema, kalenda hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo itawezesha wasimamizi wa elimu kufanya usimamizi, ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wa mitaala kwa urahisi.
Pia kuwapa fursa wanafunzi wanaohama kutopoteza au kurudia baadhi ya mada ambazo zingeweza kuwa zimeshafundishwa kabla au baada.
Aidha, kalenda ya utekelezaji wa mitaala imeandaliwa kawa kuzingatia muhtasari wa masomo na idadi ya wiki ya masomo katika mwaka ili kuweka mpangilio na mtiririko wa ufundishaji na umahiri na kupangilia idadi ya vipindi kwa kila mahiri bila kuathiri idadi.
Wakati huo huo, wabunge wamepata fursa ya kuelezwa umuhimu wa kalenda za utekelezaji wa mtaala ambao ni kuwaongoza walimu wa somo kuandaa mpango wa ufundishaji, kuwawezesha wanafunzi kukuza umahiri uliobainishwa kwenye mtaala kwa kuzingatia muda ulioelekezea katika kalenda.
Vile vile, kalenda za utekelezaji wa mtaala itawaongoza walimu kufanya upimaji wa ufundishaji kwa kuzingatia maudhui yaliyoelekezwa kufundishwa katika kalenda ya mwaka na kuwaongoza wapimaji wa watahini kuandaa mitiani inayoendana na mtiririko wa ufundishaji.