Waziri Bashungwa: Tutaanza na nyumba za walimu, mengine mazuri yatafuata

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI imesema bajeti inayokuja itaweka kipaumbele suala la nyumba za walimu pamoja na maboresho mengine ili kuongeza ufanisi zaidi katika Sekta ya Elimu nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo alipotembelea kuona baadhi ya miradi inayoendeshwa na kujua uendeshaji wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) mkoani Pwani

"Ni kipaumbele na huo ndiyo mlengo ambao Rais angependa twende nao licha ya rasilimali kuwa ndogo.Hayo yatakuwa kwenye bajeti zijazo ili kuwapunguzia changamoto ya nyumba za walimu hapa nchini,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Amesema, Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Chama cha Walimue Tanzania (CWT) itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la upandishaji madaraja, lakini kipaumbele kikubwa kwa sasa ni nyumba za walimu.

Amesema,Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatafuta fedha kwa wafadhili ndani na nje ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kutatua changamoto za walimu nchini.

"Pia Mheshimiwa Rais anataka shule kongwe ziendelee kunoa vipaji toka shule mbalimbali kwa kupata rasilimali watu na fedha, ukarabati mkubwa ni kwenda kwenye dhamira ya Rais shule kongwe zirudi kwenye ubora wake kama zamani.

"Jukumu la Serikali ni kufanya maboresho ili wanafunzi waendelee kusoma na kufanya vizuri. Kibaha sekondari inaonekana vizuri kama Rais alivyotaka ambapo ilipatiwa shilingi bilioni 1.1 za ukarabati ili kuona heshima ya shule kongwe inarudi,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi amesema kuwa shirika hilo mbali ya kupata baadhi ya mafanikio lakini kuna changamoto ambazo zinalikabili ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ambayo imejengwa zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Amesema kuwa, changamoto nyingine ni mchakato wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi ambayo iko chini ya shirika hilo kwenda Wizara ya Afya ambapo watumishi kutokana na miundo wanashinda kupandishwa vyeo kutokana na kutumikia sehemu mbili kwa wakati mmoja.

Amesema, wanaishukuru serikali kupitia mradi wa fedha za shule kongwe ambapo wao walipata fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.1 ambapo ukarabati umeufanya shule ya sekondari Kibaha kuwa kwenye mazingira mazuri.

wanafunzi wa shule ya Kibaha sekondari Abdulkarim Masa alisema kuwa wanatoa ahadi ya kufanya vizuri ambapo wanamuahidi kuwa watapata daraja la kwanza tu na hakuna mwanafunzi atakayefeli.

Naye Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Tumbi Robert Jani alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news