NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa nchini kuwajibika na kutumia wajibu wao katika kutekeleza mikakati ya wizara kufikia malengo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha leo Februari 25,2022. (Picha zote na Munir Shemweta-WANMM).
Aidha, amewataka Makamishna hao kuwapangia majukumu kwa malengo maafisa walio chini yao na kufuatilia kazi wanazowapa mara kwa mara.
Dkt. Mabula amesema hayo leo Februari 25,2022 wakati akifungua kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
‘’Yapo malalamiko ya lugha zisizofaa kwa wateja, hii haikubaliki fuatilieni hili na kulikemea vikali na kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma katika majukumu yenu ya kila siku,’’ amesema Dkt.Mabula.
Aidha, amewataka katika utekelezaji mpango mkakati wa wizara wazingatie vipaumbele vya Serikali hususan maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akizungumza kwenye kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha leo Februari 25, 2022.
Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, Waziri wa Ardhi amewataka Makamishna wa ardhi Wasaidizi wa mikoa kuwa wabunifu katika njia za kukusanya mapato.
‘’Suala la mtandao kutopatikana muda mwingi linaonekana kuwa kikwazo katika ukusanyaji maduhuli, lifanyieni kazi,’’ amesema Dkt.Mabula.
Waziri Dkt. Mabula pia amehimiza kuongezwa kwa kasi ya umilikishaji ardhi kwa wananchi na kuwataka Makamishna hao na wakuu wa idara kuweka malengo kwa kila ofisa mwenye taaluma ya ardhi kuandaa hati.
Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha leo Februari 25,2022.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amesema, baada ya kuteuliwa katika nafasi ya Katibu Mkuu alifanya ziara kwa baadhi ya mikoa na kubaini changamoto kadhaa alizozitaja kuwa ni pamoja na kutofikiwa malengo ya ukusanyaji kodi ya ardhi pamoja na baadhi ya halmashauri kutohudumia idara za ardhi kwa madai ya idara hizo kuhamishiwa wizarani.
‘’Nimeanza kuchukua hatua ili kutatua changamoto hizo ambapo tayari nimetoa maagizo mbalimbali kwenye mikoa na menejimenti ya wizara na ni matarajio yangu kikao kazi hiki kutaibua suluhisho la changamoto hizo,’’ amesema Dkt. Allan Kijazi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akizungumza kwenye kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa mkoani Arusha leo Februari 25,2022.
Kwa mujibu wa Dkt. Kijazi, Wizara ya Ardhi imekuwa ikinyooshewa vidole na wananchi kwa masuala ya ukiukwaji wa haki za wananchi na kuchafua taswira ya wizara na kutaka watendaji wa sekta ya ardhi kujitafakari na kujisahihisha kwa kutimiza wajibu ili kuondoa dhana hiyo.
Aligusia pia mpango wa urasimishaji makazi holela na kueleza kuwa, ni matarajio yake kupitia kikao hicho, washirikia wake wataibuka na mkakati wa uelekeo wa wizara katika kupanga miji sambamba na usimamizi wa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 50 zilizotolewa kwa ajili ya mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi maarufu kama KKK.