NA FRESHA KINASA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maluum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima amepongeza juhudi za mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania la mkoani Mara hatua ambayo amesema ina tija katika kuiwezesha Serikali kutokomeza vitendo hivyo kwa maendeleo ya Taifa.
Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania (katikati) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima.
"Shirika mmeonesha kazi nzuri ya kizalendo katika kushirikiana na Serikali kupambana na ukatili, mabinti hawa bila huduma yenu wengine wangekuwa wameshaolewa na kuzaa na kupoteza tumaini la kufikia ndoto zao, wengine wangekuwa wamefariki kutokana na kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, kupata ulemavu, lakini ni Jambo jema na la faraja leo mnatumaini la kufikia ndoto zenu mkiwa katika kituo hiki, someni kwa bidii na kuwa na malengo ili kwa baadaye muoneshe mfano kwa jamii yenu na taifa pia,"amesema Waziri Gwajima.
Ameongeza kuwa, Jamii haipaswi kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wa kike kwa kuwaozesha na kuwakeketa kwani wanamanufaa makubwa kwa maendeleo ya jamii na taifa wakiwezeshwa kielimu. Ambapo pia ameviomba vyombo vinavyosimamia sheria kuwawajibisha kikamilifu kwa kuwapa adhabu kali wanaobainika kuhusika kufanya vitendo vya ukatili.
Pia, Waziri Gwajima amewataka wasichana wanaohifadhiwa katika kituo hicho kutumia karama zao wakiwa katika umri mdogo kutengeneza uchumi bora katika maisha yao na Serikali itaendelea kuwafuatilia kwa karibu katika kuhakikisha wanafika mbali zaidi.
Aidha, Waziri Gwajima ameitaka jamii kuwasomesha watoto wa kike na kuwaandaa kuja kuwa watumishi na viongozi wa Taifa la kesho, huku akisisitiza jamii kuachana na mila potofu zenye madhara. Na pia akahimiza juhudi madhubuti ziendelee kufanywa na kila mwananchi kwa nafasi yake kumaliza ukatili kwa kuwafichua wahusika na kuwaripoti katika vyombo vya sheria.
Ameongeza kuwa, shirika hilo linaendelea kuwapa hifadhi wasichana waliopo katika vituo vinavyomilikiwa na shirika hilo, utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia kwa kushirikiana na Ofisi za Madawati ya Jinsia, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii katika Kituo cha Nyumba Salama Mugumu na Butiama sambamba na kuwaendeleza kielimu wasichana katika vituo hivyo ili wafikie ndoto zao.
Waziri Gwajima akiagana na wacheza ngoma ya litungi mara baada ya kufanya ziara katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Butiama mkoani Mara.