Waziri Dkt.Mabula: Kinachosemwa kufanyika huko Kibaha (Pangani) ni kitu kipya kwangu

NA DISMAS LYASSA

NI siku kadhaa zimepita tangu Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mjini mkoani Pwani, Mheshimiwa Sara Msafiri kufanya mkutano na wakazi wa Mitaa ya Mkombozi, Lumumba na Kidimu, Kata ya Pangani wilayani humo na kuwataka aidha waondoke ama walipe shilingi 2,500 mita za mraba ili wapimiwe na kumilikishwa maeneo wanayoishi kwa maelezo kuwa sio yao bali ni mali ya Serikali, wao ni wavamizi.

Eneo hilo lina wakazi zaidi ya 32,000 na nyumba zaidi ya 8000, lina shule za msingi na sekondari za Serikali, ofisi za Serikali na wafanyakazi walioajiriwa na Serikali wakiwamo maofisa watendaji, maofisa maendeleo, maofisa mifugo na wengine wengi.

Aidha hivi karibuni Serikali ilitoa sh.milioni 250  kujenga kituo cha afya kitakachokuwa na uwezo sio tu wa kutibu wagonjwa na kuondoka, pia kulaza na upasuaji. Ujenzi unaendelea.

NINI HATMA NYUMBA 8000 ZENYE WAKAZI ZAIDI 32000?

Licha ya kuwepo maendeleo hayo yanayochagizwa na Serikali, mkuu wa wilaya katika mkutano huo pamoja na mambo mengine alisema, “Wakazi wote wa mitaa ya Mkombozi, Lumumba na Kidimu ni wavamizi. Hivyo mnatakiwa kulipia Tsh2500 kwa mita za mraba ili muweze kupimiwa na kurasimishwa. Kama mtu hawezi kulipia aondoke, atafute ambako atanunua bei rahisi".

Tafsiri yake ni kwamba kama mtu ana eneo dogo lenye ukubwa wa 20 kwa 20 anapaswa kulipia 1milioni. Kauli hii ya Mkuu wa wilaya imesababisha taharuki miongoni mwa wakazi, wengi wakiamini nyumba zao zikabomolewa hawana fedha hizo.

Wakazi wa eneo hilo wengi wao ni wa hali ya chini kiasi kwamba hata Serikali ililazimika kuwasambazia umeme wa bei rahisi wa mradi wa vijijini (REA) wa shilingi 27,000 huku wengine wakiingiziwa ule unaoitwa umeme tayari ambao gharama yake ni shilingi 5000 yaani unawekewa kifaa cha taa na chenye sehemu za kuingiza chaja ya simu, radio nk.

MAJIBU YA WAZIRI WA ARDHI, DK MABULA KUHUSU TSH2500

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula (pichani) akizungumzia sakata hilo katika mahojiano yetu alisema hana taarifa nalo na hafahamu nani hao waliopitisha jambo hilo na kwa mamlaka ya nani, ameahidi kufuatilia.

Alipofafanuliwa kuwa agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya, alisema “Wizara ya ardhi ndiyo yenye dhamana na masuala yote ya ardhi hapa nchini, sio zaidi. Sijawahi kama waziri ama wizara yangu kuagiza wala kutoa maelekezo kwa wakazi wa mitaa hiyo watozwe shilingi 2500 kwa mita za mraba”.

Waziri huyo anasisitiza kuwa, “Hakuna mwenye mamlaka ya kupanga au kutoa miongozo yoyote ya ardhi ikiwemo ya gharama zaidi ya Wizara ya Ardhi, hiki kinachosemwa kufanyika huko Kibaha ni kitu kipya kwangu”.

HISTORIA YA ENEO TAJWA

Wenyeji wanasema eneo hili lilikuwa mali ya Wizara ya Ardhi kupitia mradi wa mifugo walioupa jina la Mitamba ambao kwa bahati mbaya kwa miaka mingi mno ‘umekufa’, hivyo kusababisha wananchi kuingia na kuanza kuishi.

Mwaka 2012 Serikali ililigawa eneo hilo katika sehemu mbili, eneo ambapo wananchi hawaruhisiwi kuishi, na eneo ambalo wananchi wameruhusiwa kuishi huku halmashauri ikiagizwa na Wizara ya Ardhi kuwapimia na kuwaramishia. 

Katika eneo hili lililoruhusiwa watu kuishi ndiko wanakoishi wananchi hao zaidi ya 32,000 ambao sasa wanatakiwa kulipia shilingi 2,500 kwa mita za mraba au la wavunje nyumba zao waondoke.

Julai mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi, alifanya mkutano na wananchi wa Kata Pangani, pamoja na mambo mengine aliiagiza halmashauri ipime eneo hilo na kurasimisha. 

Lukuvi hakuagiza halmashauri iwatoze wananchi shilingi 2500. Pia aliagiza maeneo yatakayoonekana yapo wazi yachukuliwe kwa ajili ya huduma za jamii.

Waziri Dkt.Mabula akaongeza kuwa, “Bei elekezi ya Serikali kupima viwanja ni sh.130,000, nitakapokuwa ofisini Dodoma tarehe mbili, nitafuatilia hili ili nione limekaaje”. Waziri alisisitiza kuwa ni wizara yake ndio yenye dhamana ya masuala yote ya ardhi ikiwemo kupanga bei na gharama, sio taasisi au mtu mwingine yeyote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news