NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ametaja mambo mawili ambayo amedai yanamnyima usingizi tangu ateuliwe kuiongoza wizara hiyo.
Mheshimiwa Waziri Masauni ametaja mambo hayo kuwa ni mauaji yanayotekelezwa na baadhi ya watu nchini pamoja na baadhi ya askari kufanya vitendo kinyume na maadili.
Mhandisi Masauni amesema hayo Februari 10, 2022 baada ya kushuhudia onesho la medani za kivita lililoandaliwa na askari wanaotarajia kuhitimu kozi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi katika kambi ya kivita ya Kambapori iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
“Kuna vitu viwili vinanikosesha sana usingizi, jambo la kwanza matukio ya mauaji mengi tangu nakabidhiwa hii nafasi mara unasikia kachinjwa mtu huko.
"Jambo la pili ni askari wachache ambao wanatia doa Jeshi la Polisi wanaofanya vitendo kinyume na maadili,” amesema Mheshimiwa Waziri Masauni.
Mhandisi Masauni aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Januari 8, 2022 baada ya Rais Samia kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Nabii Dkt.Joshua
Wakati huo huo Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amemtia moyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni na kumshauri aendelee kumtanguliza mbele Mungu katika majukumu yake ya kila siku, kwani changamoto anazokabiliana nazo mwenye jawabu ni Mungu pekee.
Nabii Dkt.Joshua ameyasema hayo leo Februari 11, 2022 makao makuu ya Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yaliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro wakati akitoa taarifa rasmi ya ujumbe ambao amepewa na Mungu katika Taifa letu kuhusu mauaji ambayo yanaendelea tangu Januari hadi Februari, 2022.
Pia Nabii Dkt.Joshua amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhadisi Hamad Masauni kwa kazi nzuri ambayo anafanya, ingawa amesema juhudi zake zinatatizwa kwa kukosa watu sahihi.
"Ni kweli vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa sana. Hasa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mhandisi Hamad Masauni) tumemuona anawajibika sana,na kwa kweli Mungu ambariki na Mungu ambariki Mama kwa kuona kuwa anaweza kumsaidia.
"Lakini amekosa watu sahihi, wa kumtia moyo na kumuunga mkono katika kazi anayoifanya. Jukumu letu sasa, mimi kama Nabii, Mungu ameniambia kuwa, nichukue hatua ya kulitahadharisha Taifa, kwanza viongozi wenye dhamana waanze kumtafuta Mungu kila mtu binafsi kwenye dhamiri yake, kwa sababu mamlaka hizi zinawekwa na Mungu,"ameongeza Nabii Dkt.Joshua.
Amefafanua kuwa, "Daudi alipoona hali mbaya ya Kitaifa alimlilia Mungu na Mungu alilipona nchi yake, kwa hiyo rai yangu ya kwanza ni viongozi wenye mamlaka kumlilia Mungu kwa sababu nina hakika ni wazalendo. Na kazi kubwa ambayo mama yetu anafanya ni tishio kubwa kwa watu wengi ambao wana uchu wa madaraka.
"Kwa hiyo, sisi watumishi wa Mungu tutasimama, mimi binafsi na kanisa langu tumeitisha maombi ya siku 121 kwa ajili ya kutokomeza hii roho ili isistawi kwenye Taifa kiasi cha kuwafikia watu wabaya na kuwaletea maslahi maovu kwenye Taifa letu.
"Tunayo maombi ya siku 121 kwa ajili ya kumuinua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampiganie na kuweza kumpa nguvu na kuweza kutimiza majukumu yake, halafu pili Mungu aweze kumuondolea watu ambao si sahihi wanaomzunguka ambao wanasubiri siku moja wamsaliti. Na maombi yetu nina hakika kuwa yatafanikiwa.
"Lakini ni muhimu wajibu huu uwafikie viongozi wenye dhamana ya Taifa letu, kumtafuta Mungu kwa sababu nchi yetu imejengwa katika msingi wa bila dini, lakini katika hofu ya Mungu,"amesema Nabii Dkt. Joshua.