NA JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema anatarajia kukutana na wasanii wa makundi yote katika kipindi kifupi kijacho ili kujua changamoto zinazowakabili kwenye kazi zao ili kupata ufumbuzi wa pamoja.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Februari 3, 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Jacqueline Woiso katika ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma.
Amefafanua kuwa, ili kuleta mapinduzi katika sanaa kuna haja ya Serikali kukaa pamoja na wadau ili kujua changamoto na kuzitatua kwa pamoja.
“Nitahakikisha tunakwenda kuwanyanyua na kuboresha kazi za wasanii wetu na kuziweka katika ubora wa kimataifa kwa kushirikiana nao ili wafaidike na kazi zao,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na Multichoice Tanzania kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuweza kufanikisha azma ya Serikali ya kutoa ajira na kuboresha maisha ya wasanii hapa nchini.
Ameipongeza Kampuni ya Multichoice Tanzania (DSTV) kwa kurusha maudhui ya kitanzania hususan Muziki na Filamu ambayo yameleta manufaa kwa wasanii.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo, ameahidi ushirikiano wa karibu na Wizara katika kuhakikisha sanaa inakuwa na wasanii wanapata kipato kutokana na kazi zao.
Awali, Mhe. Mchengerwa katika hotuba yake aliyoitoa kwenye tamasha la utoaji wa tuzo za muziki na ugawaji wa mirahaba kwa wasanii hivi karibuni alitoa wiki tatu kwa watendaji wa wizara yake kutengeneza App ya “Ongea na Waziri” ambayo ina lengo la kuwawezesha wadau wa sanaa, michezo na utamaduni kuongea moja kwa moja na wadau hao badala ilivyokuwa.
Tags
Habari