NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro awasimamishe kazi maafisa wa Polisi wa Mtwara na Kilindi ili kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.
Ameyasema hayo leo Februari 4, 2022 baada ya kuunda timu maalum ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi mkoani Tanga.
“Viongozi hawa wanapaswa wakae pembeni, watahojiwa na hii timu wakiwa nje ya ofisi,” amesema Waziri Mkuu na kuwataja maafisa hao kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mtwara (RCO) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara cha eneo alilofia mfanyabiashara Mussa Hamisi Hamisi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Greyson Mahenge anayedaiwa kujinyonga.
Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kilindi na Afisa Upelelezi wa Wilaya nao pia wakae pembeni kupisha uchunguzi.