NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaangalia utaratibu utakaofaa kuhusu suala la uhifadhi katika eneo la Loliondo lililopo kwenye wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
"Katika mjadala wetu wa leo, mmetoa maoni nasi tumeyapokea. Bado Serikali inayaangalia maslahi mapana ya umma. Tutawashirikisha pia ni lipi lina maslahi mapana kwa Watanzania."
Ametoa kauli hiyo Februari
14, 2022 wakati akizungumza na wadau wa uhifadhi kwenye kikao
kilichofanyika Wasso-Loliondo. Amesema Serikali imepokea maoni
waliyoyatoa, yatayojumuishwa na kuyawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema alichoenda
kufanya leo ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na wabunge kwa Serikali
kupitia Mwenyekiti wa Kamati wa Maliasili na Utalii iliyoielekeza
Serikali iende katika maeneo ya Loliondo, Ngorongoro na Sale na
kuzungumza na wananchi. Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa Uhifadhi, katika kikao kilichofanyika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Waso, Loliondo wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha.
“Kama ambavyo Mheshimiwa
Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza lazima tuimarishe utalii na
kuhakikisha wananchi wanashirikishwa, Waheshimiwa wabunge ambao ndio
wawakilishi wametoa maoni yao ikiwemo kushauri suala la ushirikishwaji
na ndio maana leo nimekuja hapa kuwasikiliza”.
Waziri Mkuu
amesema wote tunatambua kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka ndani
ya hifadhi ambapo tusipotafuta suluhisho la kudumu hifadhi zetu
zitaathirika. “Sisi sote tunatambua eneo hili ni la utalii, lazima
tufike mahali tuamue kama tunataka utalii au la," amesema. Baadhi ya wakazi wa Waso, Loliondo wilayani Ngorongoro na wadau wa uhifadhi wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao, Februari 14, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu amesema amefarijika kusikia kwamba wachangiaji wote waliozungumza hakuna aliyesema ardhi ni yao. "Kati ya mambo yamenifariji, sijasikia mtu akisema ardhi yetu, ardhi yetu. Sote tunatambua kuwa ardhi iliyo ndani ya mipaka ya nchi hii ni ya umma lakini tumeikasimu kwa Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
Katika kikao hicho, wananchi wa makundi mbalimbali walipewa nafasi kutoa maoni yao wakiwemo mbunge, madiwani, malaigwanan, wanamije (batemi) na wenyeviti wa vijiji. Katika maoni yao, wengi wao walisema wako tayari kushirikiana na Serikali kuendelea kutunza rasilimali za Taifa.
Tags
Habari