Waziri Simbachawene:Fanyeni kazi kwa weledi na uadilifu

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI wa Katiba na Sheria Mhe.George Simbachawene amewasihi Mawakili wote wa Serikali wanaohusika na Uendeshaji wa Mashtaka kutekeleza wajibu wa kazi zao kwa ufanisi, weledi, uadilifu na uzalendo mkubwa.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo juu ya makosa ya mtandao kwa Mawakili wa Serikali yanayofanyika katika ukumbi wa Chuo cha VETA mjini Morogoro kuanzia tarehe 21 hadi 25 Februari,2022.

Alisema, mara kwa mara Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa akizungumzia suala la kesi na Upelelezi kuchukua muda mrefu wakati mashauri yapo mahakamani na hivyo ameahidi kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka kusaidiana naye kutatua changamoto zinazopelekea kuwepo kwa changamoto katika jukumu la kuratibu Upelelezi.

Mhe. Simbachawene alisema yapo malalamiko ya watu kubambikiwa kesi na Upelelezi kuchukua muda mrefu wakati shauri limeshafunguliwa mahakamani na kuwataka Mawakili kwa idhini waliyopewa na Mkurugenzi wa Mashtaka kutatua changamoto kwa kuratibu upelelezi.
Alisema akiwa Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria ataendelea kushirikiana na Wizara zingine, Wakuu wa Taasisi pamoja na wadau wa Maendeleo kuhakikisha utamaduni wa kutoa elimu endelevu kwa wadau wote muhimu wa Haki Jinai ili kuhakikisha lengo la kudhibiti Uhalifu linatumia.

Alisema katika mazingira tuliyonayo Sehemu kubwa ya uhalifu unapangwa na unatekelezwa kwa njia ya mtandao kupitia vifaa wezeshi vya mawasiliano kama vile simu na kompyuta ingawa changamoto zake zinaathiri mila,desturi na tamaduni.

"Sote tunashuhudia namna makosa ya jinai kwa njia ya mtandao yanavyoshamiri katika jamii yetu. Makosa kama vitisho kwa njia ya mtandao, usambazaji wa taarifa za uongo, usambazaji wa picha zenye maudhui ya ngono na Uhalifu kwa njia ya mtandao yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika jamii ukilinganisha na miongo miwili iliyopita kutokana na matumizi makubwa ya Mfumo na vifaa vya mawasiliano ambayo kimsingi ndiyo maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Alifafanua kuwa makosa ya kimtandao hayaishii tu katika matukio ya kimtandao kama vile utakatishaji fedha, rushwa, ugaidi, kujipatia mali au fedha kwa njia ya udanganyifu, kujihusisha na dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu akimkaribisha mgeni rasmi alimshukuru kwa kukubali kufungua mafunzo hayo aliwataka washiriki kutumia vizuri elimu watakayoipata katika kuboresha utendaji kazi na kuwafundisha kuwarithisha wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki.
Mafunzo ya juu ya sheria ya makosa ya mtandao, upelelezi na uendeshaji kesi dhidi ya Makosa ya mtandao kwa Mawakili wa Serikali yanafanyika katika chuo cha VETA mjini Morogoro kuanzia tarehe 21 hadi 25 Februari, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news