Waziri wa Fedha awashirikisha Global Fund hitaji muhimu kwa Tanzania

NA BENNY MWAIPAJA-WFM

WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameuomba Mfuko wa Dunia (Global Fund), kuisaidia Tanzania Vifaa Tiba ili kwenda sambamba na juhudi za Serikali za kujenga miundombinu ya afya kwa kasi ili kuboresha masuala ya tiba kwa wananchi.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika wa Global Fund Bw. Linden Morrison aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi ambapo wamejadili masuala kadhaa muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisalimiana na Mkuu wa Idara ya Afrika wa Mfuko Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu Bw. Linden Morrison, alipomtembelea na kufanya mazungumzo naye katika Ofisi za Hazina, jijini Dar es Salaam.

“Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza rasilimali kubwa katika ujenzi wa Zahanati, vituo vya afya na Hospitali ambazo zimejengwa kwa kasi kila mahali nchini lakini changamoto kubwa iliyopo na ambayo tungeomba mtusaidie ni vifaa tiba vya kisasa vitakavyoiwezesha Serikali kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi” alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameilekeza Wizara ya Fedha na Mipango kutafuta rasilimali fedha itakayotumika kwa ajili kununua vitendea kazi vitakavyokuwa na hadhi ya majengo ya kisasa yanayojengwa hivi sasa na kuwafanya wananchi wapate huduma bora za afya karibu na maeneo yao.

Aidha, Dkt. Nchemba aliushukuru Mfuko huo wa Dunia kwa kutoa msaada wa dola za Marekani milioni 721 zitakazotumika kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19 zitakazotumika katika kipindi cha miaka 3 kuanzia Januari mwaka 2021 hadi Desemba mwaka 2023. Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb),( wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu uliiongozwa na Mkuu wa Idara ya Afrika Bw. Linden Morrison (wa tatu kushoto) baada ya kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Kamishna wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Japhet Justine, Kamishna wa Fedha za Nje Bi. Sauda Msemo, kutoka kushoto ni Afisa Dawati wa Global Fund wa Wizara hiyo Bi. Mukajungu Kamuzora na Bw. Nelson Msuya, Mwakilishi wa Global Fund-Tanzania. (Picha na Wizara ya Fedha na MIpango-Dar es Salaam).

Aliushukuru pia Global Fund kwa kutaka kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii wa kimatibabu ambapo watu mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia watakuja nchini kupata matibabu na pia kuwa sehemu ya utalii huo wa tiba baada ya kuimarika kwa mifumo ya utoaji wa huduma ya matibabu itakayokwenda sambamba na uwepo wa Vifaa Tiba vya kisasa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Afrika wa Global Fund Bw. Linden Morrison aliipongeza Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wake katika kupiga vita maradhi ya Kifua Kikuu, Malaria na Ukimwi pamoja na namna ilivyokabiliana na ugonjwa wa Uviko 19 kwa umahili mkubwa.

Aliahidi kuwa Mfuko wa Dunia utaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na magonjwa hayo hapa nchini kwa kuelekeza rasilimali fedha kwa ajili ya kununua dawa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma ya afya ikiwemo kuboresha mifumo ya utoaji huduma ya Bohari ya Dawa (MSD) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba hapa nchini (TFDA).

Tangu Mfuko wa Dunia (Global Fund) uanze kushirikiana na Tanzania kukabiliana na maradhi ya Kifua Kikuu, Malaria na Ukimwi mwaka 2002 hadi sasa, Mfuko huo umetoa msaada wa dola za Marekani bilioni 1.9.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news