Allawi Foundation yafanya jambo kufanikisha kumbukizi ya Shehe Mudhihir

*Yaungana na waumini mkoani Pwani kutoa ng'ombe 

NA ROTARY HAULE,

TAASISI ya Allawi Foundation iliyopo Mjini Kibaha imeungana na waumini wa dini ya Kiislamu waliopo mkoani Pwani kwa kutoa msaada wa ng'ombe mmoja kwa ajili ya kufanikisha Maulid ya kumbukizi ya aliyekuwa Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Mudhihir Lipambila.
Shehe Mudhihir alifariki Mjini Kibaha ambapo mpaka sasa ametimiza miaka miwili tangu alipofariki na kwamba Maulid yake inafanyika April 1,2022 kiwa ni sehemu ya kumbukizi ya kifo chake.

Hafla ya makabidhiano ya ng'ombe huyo imefanyika leo katika msikiti wa Shehe Mudhihir baina ya wawakilishi kutoka Taasisi ya Allawi Foundation, familia na wananchi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi ng'ombe huyo kwa niaba ya mkurugenzi wa taasisi hiyo, Abubakar Allawi mwakilishi, Jeremiah Komba (Shungu), amesema kuwa Allawi Foundation ipo katika kusaidia jamii bila ubaguzi.
Komba amesema kuwa, Allawi Foundation inatambua umuhimu wa aliyekuwa shehe huyo wa Mkoa wa Pwani kwa kuwa alikuwa mtu wa kuunganisha jamii katika nyanja zote ndio maana imejitoa kufanikisha Maulid yake.

"Tumekuja hapa kumwakilisha mkurugenzi wetu Abubakar Allawi kukabidhi ngombe huyu kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya Maulid ya Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani tangu afariki miaka miwili iliyopita,"amesema Komba.

Komba amesema kuwa, pamoja na mambo mengine lakini Shehe Mudhihir enzi ya uhai wake alimfundisha Allawi katika madrassa iliyokuwa msikitini hapo na kwamba kutoa msaada wa ng'ombe huyo ni sehemu ya kurudisha heshima kwa mwalimu wake.

Kwa upande wake kiongozi wa familia ya Shehe Mudhihir na mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mailimoja Yassin Mudhihir, ameishukuru Taasisi ya Allawi Foundation kwa kutoa msaada huo.
Yassin ,amesema kuwa kitendo cha Taasisi hiyo kuungana na familia hiyo juu ya kukamilisha Maulid ya Shehe huyo ni mfano wa kuigwa katika jamii na hata Taasisi nyingine.

"Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwalimu Abubakar Allawi kupitia Taasisi yake ya Allawi Foundation kwa msaada huu mkubwa wa ng'ombe ambao utasaidia kukamilisha Maulid ya mzee wetu hapo kesho ,tunaomba aendee kutusaidia siku nyingine bila kuchoka,"amesema Yassin.

Nae mjukumu wa Shehe huyo Hafidh Muhidhir,amesema utaratibu wa Maulid utakuwa endelevu kwakuwa wanafanya hivyo kuenzi yale ambayo Shehe alikuwa anayafanya.
Amesema Shehe Mudhihir enzi ya uhai wake alianzisha utaratibu wa kufanya Maulid kila mwaka na kwamba wao kama familia lazima waendelee kuenzi utaratibu huo kila mwaka.

Hafidh,amesema Taasisi ya Allawi Foundation imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii na tayari mwaka huu wametoa ng'ombe kwa ajili ya kukamilisha Maulid hiyo ambapo ameomba kuendelea kushirikiana kila mwaka kumuenzi Shehe huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news