NA FRESHA KINASA
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Odello Otieno mkazi wa Kitongoji cha Nyarandi Kijiji cha Wamaya Kata ya Kirogo Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara amefariki dunia kwa kusombwa na maji wakati akijaribu kuokoa ng'ombe wake katika Mto Mori uliopo katika eneo la Wamaya wilayani humo.
Akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya barabara inayotekelezwa na TANROADS na TARURA wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Jumaa Chikoka amefika eneo la Mto Mori leo Machi Mosi, 2022 na kukuta wananchi wakifanya juhudi za kutafuta mwili wa marehemu ambaye amefariki akiwa katika juhudi za kuokoa ng'ombe wake aliyesombwa na maji ya mto huo.
Aidha,ng'ombe aliopolewa akiwa amekufa huku mwili wa marehemu ukiendelea kutafutiwa na wananchi hao.
Wakizungumza na DIRAMAKINI BLOG eneo la mto Mori wakazi wa kijiji hicho wameiomba Serikali kuchukua juhudi za haraka na makusudi kuwajengea daraja ambapo walisema mto huo umekuwa tishio kwa usalama wao hasa nyakati za mvua ambapo wananchi hulipa fedha shilingi 2, 000 ili kuvushwa kwa mtubwi.
"Tunaiomba Serikali yetu ifanye hima kujenga daraja eneo hili la mto Mori. Mto huu umeshapoteza maisha ya watu na pia bado kuna shida kubwa ya kuvuka. Mathalani mtu huyu amefariki dunia muda si mrefu alikuwa na mfugo wake akijaribu kuokoa na yeye pia amesombwa pamoja na ng'ombe wake, hii inasikitisha sana.
"Mtu akitaka kuvuka lazima alipe shilingi 2,000 ndipo avushwe kwa mtumbwi Serikali isikie kilio chetu tunaiomba sana,"amesema Chuki Eliachim.
Justine Nyasebe ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Kirogo ambapo amesema kwamba, ndani ya kata hiyo kuna mito miwili ambayo ni mto Mori na mto Wamaya na nyakati za mvua mito hiyo imekuwa ikileta adha kubwa kwa wananchi kuvuka na kuhatarisha usalama wao na ameomba Serikali kutafuta mwarobaini wa kudumu kuwanusuru wananchi wa kadhia hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wananchi katika eneo hilo, amewahakikishia wananchi hao kuwa serikali imetoa fedha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Mori na kwamba mkataba wa kusaini ujenzi wa daraja hilo utafanyika ndani ya wiki hii.
Chikoka ameongeza kuwa, ujenzi wa daraja la Mto Mori ukikamilka utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi ikiwemo kuwahakikishia usalama wao, kuokoa fedha wanazotumia kulipa ili wavushwe kwa mtubwi pamoja na kufungua fursa za kiuchumi ndani ya wilaya hiyo.
Huku pia akiwaomba wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza ndani ya wilaya hiyo kupitia fursa ya kilimo, viwanda pamoja na uvuvi.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi wilayani humo kushiriki kutunza miundombinu ya barabara inayojengwa kwa fedha nyingi na serikali kusudi zidumu kwa muda mrefu katika kuwarahisishia kupata huduma za kiuchumi na kijamii.
Tags
Habari