*Mashabiki wa muziki zaidi ya 90,000 tayari wamepiga kura
NA JOHN MAPEPELE
SERIKALI kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) imeongeza muda wa siku mmoja wa kupiga kura kwa ajili ya Tuzo za Muziki 2021 ambapo awali mwisho ulikuwa leo Machi 31, 2022 saa sita usiku na sasa itakuwa hadi Aprili 1, 2022 saa sita usiku.
Aidha, siku ya utoaji wa tuzo hizo inabaki kama ilivyopangwa Aprili 2, 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Machi 31, 2022 na Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Matiko Mniko kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo amesema kuongezwa kwa siku hiyo kunatokana na wapenzi wengi wa muziki kuendelea kufurika kupiga kura katika siku hizi za mwisho.
“Siku ya kwanza tulitangaza kuwa mwisho wa zoezi la upigaji wa kura itakuwa leo tarehe 31,3,2022 saa sita usiku, lakini kutokana na watu wengi kuonyesha uhitaji katika mchakato huu tumeona tuongeze siku moja kutokana na majukumu waliyonayo ili waweze kushiriki na kuwachagua wasanii wao wanaowapenda,” amefafanua Mniko.
Amesema, toka zoezi la upigaji kura lililoanza Machi 20 mwaka huu na tayari zaidi ya wapenzi na mashabiki wa muziki zaidi ya 90000 wameshapiga kura.
Pia amesema usiku huo wa utoaji wa tuzo utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, bendi na vikundi vya ngoma.
Amesema, kesho BASATA itakutana na washiriki ili kuwapa semina ya namna ya kushiriki katika siku ya utoaji wa Tuzo za Muziki.