Bilioni 2.6/- zatolewa mkoani Pwani kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali

ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge,amesema zaidi ya Sh.bilioni 2.6 zimetolewa kwa ajili ya kuviwezesha vikundi mbalimbali vya wajasiriamali vikiwemo vikundi vya Vijana,Walemavu na Wanawake.
Kunenge amesema hayo leo wakati akizungumza na wajasiriamali mbalimbali katika uzinduzi wa Wiki ya Wanawake alioufanya katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo Kibaha -Mailimoja.

Amesema kuwa, Mkoa wa Pwani umedhamiria kuleta mabadiliko kwa kufungua fursa zaidi ili kuweza kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi ili waweze kukua kiuchumi na hata kuongeza pato la Taifa.

Aidha, Kunenge amesema kuwa kutokana na mpango huo mkoa umekuwa ukiongeza bajeti mwaka hadi mwaka ili kusudi kila vikundi viweze kupata fedha kulingana na mahitaji.

Amesema,kwa sasa mkoa upo kwenye mpango mzuri wa kuona namna ya kutoa mikopo yenye tija na kuweza kuwasaidia katika kuendeleza shughuli zao.
Kunenge amesema kuwa, moja ya mpango huo ni kuhakikisha fedha zinatolewa nyingi kwa vikundi vichache kuliko kutoa fedha ndogo kwa vikundi vingi na kusema mabadiliko hayo yataleta tija.

"Tunataka mikopo itolewe kwa viwango vikubwa kwa vikundi vichache kuliko kutoa fedha kidogo kwa vikundi vingi na hali hiyo itasaidia kuwabadilisha wajasiriamali wa Mkoa wetu,"amesema Kunenge.

Kunenge amesema, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 mkoa umetenga kiasi cha sh.bilioni 3.1 lakini Julai - Desimba tayari wamefanikiwa kutoa bilioni 2.6 kwa vikundi 440 ambapo fedha hizo zitakuwa zikiongezwa mwaka hadi mwaka.

Amesema,mafanikio hayo yanatokana na kazi nzuri ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kwamba lazima waendelee kufanya kazi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais.
Kunenge ameongeza kuwa, Rais Samia ameonesha uwezo wa wanawake katika uongozi na utekelezaji wa majukumu na hiyo inadhirisha namna ambavyo wanawake wanaweza kufanya kazi.

"Nitumie fursa hii kumpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayofanya na hakika ameonyesha uwezo wa wanawake katika kuongoza na mkoa unatekeleza sheria kwa kuwawezesha wanawake,"amesema Kunenge.
Katika hatua nyingine Kunenge,ametumia nafasi hiyo kuwaomba wajasiriamali pamoja na wanawake kujitokeza kuhesabiwa pale zoezi la Sensa litakapowadia sambamba na kusisitiza kushiriki zoezi la anuani za makazi na hata kuchanja chanjo ya Uviko-19.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri amesema,wametenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya wajasiriamali sambamba na kuwajengea uwezo Wanawake Kisiasa,Kiuchumi na Kiujasiriamali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news