Bilioni 460/- kufungua Mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI imepanga kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 460 katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuweza kuufungua kibiashara na kuchochea fursa nyingi za kimaendeleo mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, akikagua ujenzi wa Daraja la Makere lenye urefu wa mita 20 lililopo katika barabara ya Kanyani – Mvugwe (km 70.5) inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Kigoma.

Aidha, Bilioni 21 zimetolewa kwa ajili ya miradi mingine ya nyongeza ambayo itagusa jamii inayozunguka katika miradi ikiwemo ujenzi wa wa Shule, Soko, Miundombinu ya Maji Safi na Taka na Vituo cha Mabasi katika wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyovu mara baada ya kukagua hatua ya ujenzi wa barabara ya Kanyani – Kidyama – Mvugwe (km 70.5), Njia panda ya Kasulu – Manyovu (km 68.25) pamoja na eneo patakapojengwa Kituo cha Kisasa cha Pamoja cha Manyovu/Mugina (OSBP) mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Naibu Waziri huyo amezitaja barabara ambazo zinatekelezwa kwa fedha hizo ikiwa ni ujenzi wa barabara ya Njia panda ya Nduta – Kabingo (km 62.5), Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini (km 25.9), Mvugwe – Njiapanda ya Nduta (km 59.35), Kanyani – Kidyama – Mvugwe (km 70.5), Njia panda ya Kasulu – Manyovu (km 68.25) ambazo zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2023.
Kaimu Mhandisi Mshauri wa kampuni ya Afrisa anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kanyani – Mvugwe (km 70.5) kwa kiwango cha lami, Mhandisi Regnard Kaganga, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Makere (m 20), mkoani Kigoma.

“Serikali imeamua kuweka wakandarasi wengi katika mkoa huu kwa kuwa Kigoma haukuwa umefunguka kwa barabara za lami sasa zimeanza kujengwa hivyo tunawajibu kama wananchi kulinda miundombinu hii na kujiweka tayari kwa kufanya biashara na mikoa mingine ya jirani ili kujiongezea kipato,”amefafanua Kasekenya.

Ameongeza kuwa tayari wakandarasi wapo eneo la kazi kutokea Kigoma ukielekea Tabora kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Malagarasi (km 51.1) na Kazilambwa – Chagu (km 36) kwa kiwango cha lami.

Katika kufungua mkoa wa Kigoma na Katavi, Eng. Kasekenya amesema kuwa tayari mkandarasi amekwishaanza ujenzi kutokea Mpanda (km 50) kuelekea Uvinza ili kupunguza umbali wa safari ukitokea Katavi.
Mkandarasi wa Kampuni ya Sinohydro Corporation, Lui, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa sweta), wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Kanyani – Mvugwe (km 70.5) kwa kiwango cha lami, mkoani Kigoma.

“Tuna barabara tatu kubwa ambazo zinaunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa mingine ambazo ni barabara ya Kibondo, Tabora, na Mpanda na tayari wakandarasi wamekwishanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami,”ameeleza Naibu Waziri Kasekenya.

Aidha, Wakala wa Barabara (TANROADS), umekwishaanza usanifu wa kina wa barabara ya Kalela – Munzeze – Kirungu – Janda – Bukuba - Buhigwe (km 57.35), Buhigwe – Nyamugali - Muyama – Katundu (km 120) kwa ajili ya maandalizi ya kujengwa kwa kiwango cha lami.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwasimamia wakandarasi wote waliopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo ili kuhakikisha mkoa wa Kigoma unafunguka na kurahasisha shughuli za usafirishaji na mikoa jirani pamoja na nchi jirani.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, kuhusu Kituo cha Pamoja cha Manyovu/Mugina (OSBP) kitakachojengwa mpakani mwa Tanzania na Burundi, mkoani Kigoma.

“Nikuhakikishie Naibu Waziri TANROADS tuko bega kwa bega kusimamia miradi hii licha ya changamoto za mvua na zinginezo watakamilisha kwa wakati na ubora uliosanifiwa”, amesema Mhandisi Choma.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Kigoma katika ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news