*Arudishwa kundini baada ya kuomba msamaha
NA GODFREY NNKO
KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi-CCM (NEC) kinachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo kimetangaza kumsamehe na kumrudishia uanachama Bernard Membe baada ya kuandika barua ya kuomba msamaha.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo leo Machi 31, 2022 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa NEC uliofanyika chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Uamuzi huo unafikiwa baada ya mwanzoni mwa mwaka 2020 Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumvua uanachama Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje.
Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole ndiye aliyetangaza maamuzi hayo ya kamati katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.
Wakati Membe akivuliwa uanachama, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana alipewa karipio na kutakiwa kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kwa miezi 18 huku katibu mkuu mwingine wa zamani Yusufu Makamba akisamehewa.
Makada hao walihojiwa baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayejiita mwanaharakati, ambaye alikuwa akitoa tuhuma dhidi yao.
Baadaye Mwanadiplomasia huyo alitangaza kuhamia Chama cha ACT Wazalendo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2020, baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Februari 28, 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), tarehe 10 Julai 2020.
Baada ya kuhamia ACT Wazalendo, Membe alitangaza kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.
Akijiunga ACT Wazalendo Membe alisema, “Kwa hiari yangu nimeamua kujiunga katika familia kubwa ya ACT Wazalendo inayotaka mabadiliko yenye lengo la kuwanufaisha Watanzania wengi hasa wakulima, wafanyabiashara, watumishi wa serikali, wafanyakazi mbalimbali na wote wanaoitakia kheri Tanzania yetu. Nataka kupigania mabadiliko ya kweli ya hii nchi kupitia ACT na azma yangu itatimia”.
Alijikuta hivi
Hata hivyo, kuliibuka migogoro ndani ya chama hicho baada ya viongozi wa ACT Wazalendo kutangaza kumuunga mkono Mgombea Urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu licha ya Membe kuwa mgombea Urais kupitia ACT Wazalendo.
Ijumaa Oktoba 16, 2020 Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitangaza kumpigia kura mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni mjini Kigoma.
Mbali na Zitto, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad (kwa sasa marehemu) aliwahi kutangaza kuwa chama hicho kitamuunga mkono Lissu katika Urais ambapo pia Lissu pia aliwahi kutangaza kuwa Chadema itamuunga mkono Maalim Seif katika urais wa Zanzibar.
Hata hivyo Membe alisisitiza kuwa yeye ni mgombea halali wa Urais kupitia ACT Wazalendo. “Mimi Bernard Membe ni mgombea halali wa ACT-Wazalendo wa nafasi ya Urais. Na chama chetu ni kizuri kabisa ambacho nitakipeleka 28 Oktoba 2020 vizuri kabisa,”alisema.
Hata hivyo,Januari 1,2021 Mgombea huyo wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo na mshauri wa chama hicho alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho.
Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 alitangaza uamuzi huo akiwa nyumbani kwake kijijini Rondo Chiponda, Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi ambapo alisema hakufanya uamuzi huo kwa shinikizo lolote na kwamba kwa sasa atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi ya Tanzania.