*Balozi Mushy aahidi kwenda kuyafanyia kazi maono ya Rais Dkt.Mwinyi juu ya Sera ya Uchumi wa Buluu nchini Austria
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepongeza utayari wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Switzerland kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika jitihada zake za maendeleo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi Mpya wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian alipofika Ikulu jijini Zanzibar na Ujumbe wake kwa mazungumzo na kujitambulisha mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo kwa nyakati tofauti Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazunguzo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian aliyekuja kujitambulisha pamoja na Balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Didier Chassot.
Mapema akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Balozi Chen Mingjian, Rais Dkt. Miwnyi amesema kuwa, Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na nchi hiyo na kuahidi kuuendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.
Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu na nyinginezo hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amemueleza Balozi huyo wa China mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake kupitia Sera ya Uchumi wa Buluu.
Naye Balozi Chen Mingjian amemuahidi Rais Dkt.Mwinyi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono Sera yake ya Uchumi wa Buluu.
Balozi huyo wa China katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kutokana na uhusiano mzuri na ushirikiano mwema inayopata Ubalozi Mdogo uliopo Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi pia, alipata fursa ya kuzungumza na Balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Didier Chassot na kumpongeza kutokana na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia sekta ya afya, kuanzisha Bima ya Afya, utawala bora, kuijengea uwezo Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka pamoja na kuzisaidia Asasi za Kiraia (NGOs) za hapa nchini.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Switzerland kwa kusaidia juhudi za Serikali za kuanzisha Bima ya Afya hapa Zanzibar ambapo matarajio makubwa kwamba katika mwaka ujao wa fedha Bima hiyo itaanza sambamba na kusaidia vifaa katika kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19.
Nae Balozi wa Swiitzerland Didier Chassot alitoa ahadi kwa Rais Dkt. Mwinyi kwamba Serikali yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika nyanja mbali mbali ikiwemo afya pamoja na Utawala Bora.
Katika maelezo yake Balozi huyo wa Switzeland alimueleza Rais Dkt. Mwinyi hatua zinazochukuliwa na nchi yake katika kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea katika kuisaidia Zanzibar.
Balozi Didier Chassot alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuwa karibu na Asasi za Kiraia pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuziwekea mazingira mazuri Asasi hizo.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Austria, Celestine Mushy ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais akiwa tayari kuelekea katika kituo chake cha kazi nchini Austria.
Katika mazungumzo na Balozi huyo wa Tanzania nchini Austria, Rais Dkt. Mwinyi alieleza haja kwa Balozi huyo kuzitumia fursa zilizopo nchini Austria katika kuhakikisha zinainufaisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuifanyia kazi Diplomasia ya Uchumi ambayo ndio Dira ya nchi hii.
Sambamba na hayo, Balozi Mushy alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba miongoni mwa majukumu yake atakayoyatekeleza nchini Austria ni pamoja na kuhakikisha anayafanyia kazi maono ya Rais Dkt.Mwinyi juu ya Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo anatarajia yataipaisha kwa kiasi kikubwa Zanzibar kiuchumi.