>Mwalimu Deus Seif aeleza mambo yalivyo mazuri kwa upande wa walimu
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KATIBU Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Deus Seif ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja mara mbili walimu 52,000 na ongezeko la ajira za walimu kwa kipindi cha mwaka 2021.
Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifunga kikao cha Baraza la Walimu Dodoma, ambapo amesema katika ajira zilizotolewa kwa kipindi cha mwaka 2021 walimu wamepewa kipaumbele kwa kiwango cha asilimia 70.
''Kutupandishia madaraja kwa kiwango hiki siyo kazi ndogo na haijawahi kutokea tangu tupate uhuru na sehemu hiyo tumenufaika sisi walimu. Kwa kipindi hiki mnaweza kuona namna gani sisi walimu tumebebwa, ukiachilia mbali madarasa ya Covid (UVIKO-19) ambayo yanakufanya ukiingia darasani unakuta dawati lipo kiti darasa zuri lenye sakafu yote haya yanaturahisishia tendo la kujifunza na kufundisha sisi walimu,''amesema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, amewataka viongozi wa chama hicho kuwatumikia walimu ipasavyo ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuachana na tabia za kugawa wanachama.
“Imefika wakati sote tutembee pamoja, nyinyi ambao tayari ni viongozi wa wilaya na mkoa muwe faraja kwa wenzenu. Maana matatizo yote na shida zinakuwa zipo kwetu sisi viongozi kama mwalimu amekuamini amekupa kadi yake ya benki kwa ajili ya makato ya asilimia mbili, kwa nini msiwatumikie,”amehoji Katibu Mkuu huyo.
Naye Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Dodoma, Mwalimu Samweli Malechela amesema, kikao hicho cha baraza kinafanyika mara baada ya miaka miwili ambapo kinawakutanisha viongozi wa Chama cha Walimu katika ngazi za wilaya lengo likiwa ni kujadili mambo mbalimbali yanayohusu walimu.
“Kikawaida sisi kama viongozi wa mkoa wa Chama cha Walimu huwa tunakutana kwa lengo kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili walimu na kuzitatua katika ngazi za wilaya na mikoa ili yasifike Taifa,”amesema Mwenyekiti huyo wa CWT Mkoa wa Dodoma.