DP World yazindua soko la jumla mtandaoni nchini Tanzania

*Yatajwa kuwa fursa mpya ya biashara ya kidijitali nchini Tanzania na katika Ukanda wa Afrika Mashariki,kuongeza ufanisi na uhakika katika biashara za jumla kwa wafanyabiashara nchini Tanzania, kwa kuwezesha upatikanaji wa masoko kwa biashara za ukubwa mbalimbali

*Ukanda mpya wa biashara za kidijitali unaoundwa na DUBUY.com unaenda sambamba na kanda za usafirishaji ambazo DP World imejenga katika bara zima la Afrika, ikijumuisha bandari, gati na huduma za usafirishaji

NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya DP World imezindua rasmi jukwaa lake la biashara za jumla mtandaoni liitwalo DUBUY.com nchini Tanzania.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Prof. Godius Kahyarara (aliyesimama kushoto) na Naibu Balozi wa UAE nchini, Mohammad Al Bahri wakishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano kati ya TCCIA na DP World katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2022. Wanaotia saini makubaliano hayo ni Rais wa TCCIA, Paul Koyi, (aliyeketi kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dubai Trade World, Mahmood Al Bastaki.

Soko hilo la mtandaoni litawapa wafanyabiashara wa Kitanzania nafasi ya kushiriki katika masoko ya kimataifa. Jukwaa hilo pia litakuza usalama na uhakika katika biashara, kupitia bandari na mtandao wa huduma za usafirishaji zinazoendeshwa na DP World.

Jukwaa hili jipya linawezesha wafanyabiashara wa Kitanzania kuuza bidhaa za jumla za aina mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mbali na teknolojia ya hali ya juu, DUBUY.com inawapa watumiaji fursa ya kipekee ya kufaidika na miundombinu inayoendeshwa na DP World - ikiwemo Bandari ya Berbera nchini Somalia - katika kutatua vikwazo mbalimbali vya ukuaji wa biashara ya mtandaoni barani Afrika. Hii ni pamoja na uhakika katika ukamilishaji wa mauzo au manunuzi, usalama katika miamala ya kifedha, na usalama katika usafirishaji wa bidhaa.

Uzinduzi wa DUBUY.com nchini Tanzania umekuja baada ya uzinduzi wa jukwaa hilo nchini Kenya na Rwanda mnamo mwaka jana, na kuunda jumuiya ya wafanyabiashara mtandaoni inayowaunganisha zaidi ya wafanyabiashara hai 1,500.

Ujio wa DUBUY.com nchini Tanzania unathibitisha dhamira ya jukwaa hilo katika kuunda lango la kimkakati la biashara katika nchi za Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mahmood Al Bastaki, Afisa Mtendaji Mkuu wa Dubai Trade World alisema: “Dubuy.com inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani kukua na kufikia kiwango cha kimataifa kwa kuwawezesha kushiriki katika masoko mapya barani Afrika, Mashariki ya Kati na kwingineko ulimwenguni.

"Tuna furaha kubwa kutokana na kuendelea kupanua wigo wa huduma zetu katika nchi za Afrika Mashariki kufuatia uzinduzi wa jukwaa hili hapa Tanzania, nchi hii ni soko muhimu kimkakati kutokana na kasi yake ya ukuaji wa uchumi na fursa za biashara mtandaoni ambazo kwa muda mrefu hazijatumiwa ipasavyo.


"Ni matumaini yetu kuwa upatikanaji wa nyenzo hii mpya ya kidijitali utawezesha biashara za ndani kukua zaidi,”amesema.

Naye Bw. Paul Koyi, Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania amesema, “Dira ya Maendeleo ya Tanzania kufikia mwaka 2025 ni kuwa na uchumi imara, mtambuka, unaostahimili ushindani, rahisi, na unaoweza kuendana na mabadiliko ya hali ya soko na teknolojia katika uchumi wa nchi, kanda na wa kimataifa.

"Tunajua kuwa fursa kama hizi zinazotokana na ushirikiano wetu wa kimkakati na DP World na DUBUY.com zitatusaidia kufikia maono haya.

"Zaidi ya hayo, fursa hii itakuwa kiungo cha biashara nchini na kuwawezesha wafanyabiashara wa Kitanzania kushiriki kwa urahisi katika soko, na kutusaidia kufikia ukuaji endelevu. Kwa utaalam wetu wa ndani, na rekodi nzuri ya kimataifa ambayo DP World imejijengea, tunajihakikishia nafasi nzuri kama sehemu ya soko la kimataifa katika siku zijazo,"amesema.

Kuhusu DUBUY.com

DUBUY.com inayoendeshwa na DP World ni lango la biashara barani Afrika. DUBUY.com ni sehemu ya DP World, biashara ya kimataifa ya huduma za usafirishaji yenye vituo 127 vya kibiashara katika nchi 51.

Jukwaa lao bunifu la kidijitali linatoa fursa la soko mtandaoni baina ya wafanyabiashara na huduma zote za mauzo au manunuzi barani Afrika na kwingineko.

Pia wanaunganisha biashara za Kiafrika na masoko ya kikanda na kimataifa, na kuhakikisha kuwa bidhaa zinafikishwa kwa usalama, kwa uhakika na kwa wakati.

Likiwa na zaidi ya mataifa 50 na idadi ya watu ipatayo bilioni 1.3, bara la Afrika linatoa fursa ya kipekee kwa makampuni makubwa na madogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news