DPP Mwakitalu:Upelelezi mzuri ni nguzo muhimu katika utoaji wa hukumu ya haki

NA MWANDISHI MAALUM

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini, Bw. Sylvester Mwakitalu amesema upelelezi mzuri ni nguzo muhimu katika kuhakikisha kuwa hukumu inatolewa vizuri na kwamba usipofanyika vizuri wahalifu hawataweza kupatikana.

“Upelelezi usipofanyika vizuri hakuna namna Mwendesha Mashtaka ataendesha kesi vizuri. Uchunguzi na upelelezi wa mali lazima ufanyike vizuri ili kupelekea mashtaka kuandaliwa vizuri ili mhalifu asinufanike kwa mali alizozipata kwa njia ya uhalifu.

"Mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu zitafutwe, zifuatiliwe na zitaifishwe ili kuhakikisha kuwa uhalifu unakomeshwa na kuwapa taarifa wahalifu kuwa uhalifu haulipi;
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo juu ya taratibu za Kisheria za Utaifishaji Mali na Makubaliano ya Kukiri Makosa kwa Waendesha Mashtaka na Wapelelezi yanayoendelea jijini Mwanza.

Bw. Mwakitalu amesema, Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanawarahisishia Wahalifu kufanya uhalifu, kuficha na kuzitakatisha kutokana na uhalifu kufanyika katika mifumo ya kiektroniki, hivyo inabidi kutobaki nyuma na kuhakikisha Waendesha Mashtaka na Wapelelezi wanajengewa uwezo ili waweze kudhibiti uhalifu.

Amesema, ni matarajio yake kuwa mafunzo wanayoyapata yanatarajiwa kuwa na matokeo bora na kuboresha utendaji kazi. 

“Kufundisha watu sabini na tano tu siyo jambo kubwa ila ninachotaka kukipata baada ya mafunzo haya ni kuona maboresho yakitokea katika utendaji kazi na kuona namna uendeshaji wa mashtaka unavyobadilika na kuendeshwa kwa weledi na kuhakikisha kuwa majalada yanayofikishwa mahakamani yanakuwa na ushahidi unaojitosheleza kwa kuwa na mashtaka kamili badala ya kuwa na ushahidi wa kuungaunga,"amesema.
Amesema kumekuwa na changamoto na kelele nyingi na manung’uniko juu ya taratibu za Makubaliano ya Kukiri Kosa(Plea-Bargaining) kwa kuwa ni utaratibu mpya, lakini ni mzuri ambao ukitumika vema utasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa, hivyo amesema mafunzo yanayotolewa yatawezesha kuboreshwa kwa utaratibu huo.

“Nategemea mkitoka hapa kwenye mafunzo kuhusu Utaratibu wa Makubaliano ya Kukiri Kosa (Ple- bargaining) mtaenda kufanya kazi kwa weledi na pia nahitaji mjitahidi kujifunza kwa bidii ili muweze kufanya kazi vizuri katika eneo hilo,"amesema.

Amesema, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imepewa jukumu kubwa la kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu hivyo amewataka Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kufikisha ujumbe kwa wahalifu kuwa uhalifu haulipi kwa kufanya kazi kikamilifu.

Amelishukuru Shirika lisilo la Kiserikali la PAMS Foundation kwa kuona umuhimu wa kufadhili mafunzo na tafiti mbalimbali kwa watumishi wanaopambana na uhalifu.
Aidha, amewataka kuzingatia mafunzo wanayoyapata na kuyapa uzito unaostahili kwakuwa Waendesha Mashtaka na Wapelelezi ni watu muhimu katika suala zima la utoaji wa Haki Jinai.

Mkurugenzi wa Mashtaka pia alitumia nafasi hiyo Kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Juma na Mahakama ya Tanzania kwa kukubali kutoa Waheshimiwa Majaji, Mahakimu na Wasajili kushiriki katika mafunzo kwa kutoa mafunzo (mada) kwani kuwa nao ni nafasi adhimu na isiyoweza kupatikana kwa urahisi kutokana na majukumu waliyonayo na pia uzoefu walionao wanapoutoa utasaidia kurekebisha makosa yanapojitokeza.
Mafunzo juu ya taratibu za Kisheria za Utaifishaji Mali na Makubaliano ya Kukiri Makosa kwa Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kuanzia tarehe 28 Februari, 2022 hadi Machi 4 Machi, 2022 yameandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kufadhiliwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la PAMS.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news