EAC yapanua fursa za biashara na masoko,DR Congo yapewa nafasi

*Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaeleza nchi nyingine inaweza kujiunga na jumuiya hiyo iwapo itaungwa mkono na nchi wanachama

NA GODFREY NNKO

VIONGOZI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameridhia rasmi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kutokana na uamuzi huo, EAC kwa sasa inafikisha wanachama saba ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na DRC yenyewe.

Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za EAC wa 19 wa Kawaida mbao umefanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom leo Machi 29,2022 amesema kuwa,DRC kukubaliwa kuingia EAC kunaashiria tukio muhimu katika historia ya ushirikiano wa jumuiya hiyo.

DRC inapoingia EAC inafanya eneo la jumuiya hiyo kuwa na watu zaidi ya milioni 280 na uchumi wenye pato halisi (GDP) ya dola bilioni 262.

Wakati akihutubia mkutano huo wa Wakuu wa Nchi EAC, Rais Kenyatta ambaye ndiye mwenyekiti amesema kuwa, ujio wa DR Congo katika jumuiya hiyo kutaiwezesha kupata maendeleo yanayohitajika kwa kuzingatia uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.

“Leo, tarehe 29, ni siku ya kihistoria katika historia ya EAC tunapoiingiza DRC ndani ya EAC. Tayari tumezingatia na kukubaliana katika kikao chetu kilichofungwa na mkutano huo umechukua uamuzi wa kuiingiza DRC katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kukubaliwa kwa DRC kuingia EAC ni historia sio tu kwa nchi zetu bali bara letu kwa ujumla,"amesema.
Viongozi walioshiriki mkutano huo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hasan, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Paul Kagame wa Rwanda, Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bagombanza, Waziri Ofisi ya Rais Sudan Kusini, Dkt.Barnaba Marial Benjamin na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi.

Katika jumuiya hiyo, Jamhuri ya Kenya inaendelea kuongoza kwa uchumi wa pato halisi la dola bilioni 95.5, Tanzania dola bilioni 63.2 huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikishika nafasi ya tatu kwa pato halisi la uchumi wa dola bilioni 50.4.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliomba kujiunga na jumuiya hiyo tangu mwezi Februari mwaka 2021 na mamlaka husika zilikuwa bado zinapitia ombi hilo kwa kuzingatia mkataba wa kuanzishwa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Desemba mwaka 2021, wakuu wa jumuiya hiyo walipokea ripoti ya uhakiki wa utayari wa DRC kujiunga na EAC na kuwataka mawaziri wa jumuiya hiyo kuharakisha mchakato wa majadiliano ya mkataba ili kuiwezesha nchi hiyo kuwa mwanachama na kuiwasilisha mapema mwaka huu wakati wa mkutano wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Pia katika mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi uliofanyika mwaka 2021, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki alibainisha kuwa mwezi Machi, mwaka huu hatua zote za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na jumuiya hiyo zitakuwa zimekamilika.

Aidha, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa nchi ya saba kujiunga na jumuiya itawezesha kupanuka kwa mzunguko wa biashara na upatikanaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya.

Pia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itanufaika katika ukuaji wa matumizi ya bandari, jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi nchini pamoja na nchi zilizopo ndani ya jumuiya.

Taifa hilo kubwa,kupewa nafasi ya kuingia katika jumuiya itasaidia mapambano dhidi ya makundi ya waasi ambao wamekuwa wakitajwa kujificha ndani ya misitu mikubwa DRC na kuzishambulia nchi kama Rwanda na Uganda na maeneo jirani.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia mwaka 1971 hadi 1997 ilikuwa inajulikana kama Zaire. Taifa hilo linapakana na Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini katika upande wa Kaskazini, Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania upande wa Mashariki, Zambia na Angola upande wa Kusini na Bahari Atlantic upande wa Magharibi.

Ndiyo nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika kieneo, ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara, na ya 11 duniani na ndiyo nchi inayozungumza Kifaransa yenye wakazi wengi zaidi, ya nne kwa kuwa na watu wengi zaidi barani Afrika na ya kumi na tisa duniani.

Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaeleza kuwa, nchi nyingine inaweza kujiunga na jumuiya hiyo iwapo itaungwa mkono na nchi wanachama na iwapo nchi hiyo inayoomba itakuwa imetimiza masharti ya uongozi bora, demokrasia, inaheshimu sheria, inasheshimu haki za binadamu, na kwamba iwe jirani na mojawapo ya nchi wanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news