NA MWANDISHI DIRAMAKINI
TIMU ya Taifa ya Ghana imefanikiwa kufuzu kwenda kucheza Kombe la Dunia Qatar 2022 licha ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi Nigeria katika mtanange uliopigwa nchini Nigeria.
Mtanange huo wa Machi 29,2022 umepigwa katika dimba la Taifa la Abuja nchini Nigeria ambapo Ghana ilianza kupata bao la kuongoza kupitia staa anayekipiga Arsenal, Thomas Partey dakika ya 10 na baadaye Nigeria wakasawazisha kupitia mkwaju wa penalti iliyopigwa na William Troost -Ekong.
Katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0, kwa matokeo ya 1-1, hivyo Ghana imepata faida ya bao la ugenini.
Wakati huo huo, mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 Senegal wamefanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022.
Ni kufuatia kuifunga Misri kupitia mikwaju ya penati baada ya sare ya bao 1-1 kwenye mechi mbili za raundi ya kwanza na ya pili.
Mtanange huo umepigwa Machi 29, 2022 katika dimba la Stade Me Abdoulaye Wade (Stade de l'Amitie) jijini Dakar, Senegal.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo ulipigwa kwenye Uwanja wa Cairo International ambapo Misri ilishinda kwa bao 1-0 mnamo Machi 25, 2022.
Mshambuliaji na nahodha wa Misri, Mohamed Salah alikosa penati yake ikiwa ni ya kwanza kwa timu yake, wakati Sadio Mane alifunga penati ya mwisho na kuipeleka timu yake Qatar.
Senegal ambao wanashika nafasi ya kwanza Afrika kupitia viwango vya FIFA walikuwa wanahitaji kushinda angalau kwa bao mbili kufuzu, lakini haikuwa hivyo kwani dakika 120 zilimalizika kwa ushindi wa goli 1-0.
Mbele ya mashabiki zaidi ya 50,000 wakishangilia na kuzomea, Senegal walijikuta katika ugumu wa kuipita safu imara ya ulinzi ya Misri na kufanya mchezo kuwa mgumu na kuamuliwa kwa penati ambapo Senegal wamesonga mbele kwa faida ya 3-1.