Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amemkabidhi zawadi ya mfano wa meli mwanamuziki maarufu Duniani mwenye asili ya Lebanon, Maher Zain kutoka nchini Sweden anayejulikana kwa Nyimbo za Kaswida, kama sehemu ya kuhamasisha utalii hapa nchini.
Waziri Mchengerwa amemkabidhi zawadi hiyo katika tamasha la siku moja lililofanyika usiku wa Machi 12 jijini Dar es Salaam, maalum kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa vyombo vya usafiri na kukuza kipato kwa walemavu wasio ona wanaolelewa katika kituo cha Vimdat kilichoko Kisemvule jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mamia ya mashabiki wake waliofurika kuburidika na nyimbo zake kabla ya kuhitimisha tamasha hilo, mwanamuziki huyo maarufu wa Qaswida duniani aliyevalia tisheti yenye maneno (Tanzania Unforgettable) amesema uwepo wake Tanzania ni jambo asiloweza kulisahau maishani mwake kutokana na uzuri wa Tanzania na ukarimu wa watu wake.