*Rais Samia aipongeza TAKUKURU kwa kuweza kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kuitaka kujielekeza zaidi katika kuzuia kuliko kupambana na rushwa
NA GODFREY NNKO
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 1,188 katika sekta za ujenzi, maji, afya, elimu, fedha na kilimo yenye thamani ya shilingi bilioni 714.17. Thamani hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa mikataba ya kazi husika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Taasisi ya TAKUKURU kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, CP Salum Hamduni katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma leo Machi 30, 2022.
Hayo yamesemwa leo Machi 30,2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Rashid Hamduni wakati akikabidhi taarifa ya utendaji kazi ya mwaka 2020/2021 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameipongeza TAKUKURU kwa kuweza kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kuitaka taasisi hiyo kujielekeza zaidi katika kuzuia kuliko kupambana na rushwa.
CP Hamduni amesema, TAKUKURU katika kipindi cha mwaka 2020/21 ilitekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia na kupambana na rushwa kama yalivyoaiishwa katika Mpango Mkakati wake wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022.
"Miradi 966 yenye thamani ya shilingi bilioni 635.09 ilibainika kuwa na mapungufu madogo madogo hivyo, watekelezaji wake walishauriwa namna bora ya kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo kupitia vikao kazi. Miradi 222 yenye thamani ya shilingi bilioni 79.14 iliyoonekana kuwa na viashiria vya ufujaji na ubadhirifu wa fedha, uchunguzi umeanzishwa na unaendelea,"amefafanua CP Hamduni.
Kwa upande wa uchambuzi wa mifumo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ameema kuwa, jumla ya kazi za uchambuzi 683 zilifanyika kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna bora ya kuiziba mianya ya rushwa iliyobainika.
Amesema, kazi hizo zilihusu mfumo wa ukusanyaji wa ushuru wa huduma (service levy) katika halmashauri 141 nchini,mfumo wa utoaji na urejeshaji wa mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,mfumo wa utoaji wa vibali vya ujenzi katika halmashauri 102 nchini.
Pia kuna mfumo wa utoaji huduma ya mikopo inayotolewa na makampuni binafsi kwa wananchi na Mfumo wa malipo wa EPICOR katika halmashauri mbili.
"Matokeo ya chambuzi za mifumo yaliainishwa na kuwasilishwa kwenye warsha na vikao vya wadau 437, ambapo mikakati ya kuiziba mianya iliyobainishwa iliwekwa na wahusika kutakiwa kuiziba mianya hiyo.
"Mheshimiwa Rais,kutokana na kazi za uzuiaji rushwa zilizofanyika, vitendo vya rushwa ambavyo vingeweza kutokea na kusababisha ubadhirifu na ufujaji wa rasilimali za umma vilidhibitiwa, miradi ya maendeleo iliyofuatiliwa iliweza kutekelezwa kwa ubora uliokusudiwa na wananchi kuweza kupata huduma stahiki kwa wakati,"amesema CP Hamduni.
UELIMISHAJI UMMA
Katika kuhamasisha umma kushiriki mapambano dhidi ya rushwa, CP Hamduni amesema, elimu ilitolewa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa TAKUKURU. Jumla ya kazi 17,486 za uelimishaji umma zilifanyika (zikiwemo semina 3,025, mikutano ya hadhara 3,908, maonesho 357, vipindi vya redio na runinga 346; taarifa 230 zilitolewa kwa vyombo vya habari; makala 685.
Sambamba na kuimarisha jumla ya klabu za wapinga rushwa 7,334 ambapo malengo mahususi yalikuwa ni kubadili mtazamo wa wananchi kuhusiana na kuzuia na kupambana na rushwa, kuongeza ufahamu na uelewa wa wadau juu ya kampeni ya mapambano dhidi ya rushwa na kuwawezesha wananchi kuchukua hatua stahiki, kuimarisha uwezo na ufanisi wa wadau wanaoshiriki mapambano dhidi ya rushwa.
"Mheshimiwa Rais,TAKUKURU inatambua umuhimu wa ushiriki wa wananchi na wadau kwenye mapambano dhidi ya rushwa na kwa kipindi cha mwaka mmoja, kupitia programu za uelimishaji umma tumefanikiwa kuwafikia wananchi kwa njia mbali mbali ikiwemo kulifikia kundi la Vijana wa Skauti.
"TAKUKURU imefanikiwa kuanzisha ushirikiano na Chama cha Skauti Tanzania na kuunda ushirika uitwao TAKUSKA. Kupitia ushirikiano huu, tumeandaa Mwongozo wa Mafunzo, utakaotumika kufundisha vijana wa Skauti kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo husika ulikabidhiwa kwa Mlezi wa Skauti nchini ambaye ni wewe Mheshimiwa Rais mnamo Oktoba 02, 2021 siku ya Mlezi wa Skauti,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
CP Hamduni amesema, wamefanya hivyo kwa kutambua kuwa vijana walioko shuleni na hata vyuoni ni kundi kubwa (kakriban asilimia 62 ya wananchi wa Tanzania, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012).
Hivyo, ukiunganisha nguvu na vijana wa Skauti ambao wana umri wa kuanzia miaka mitano 5 hadi 26, itasaidia kujenga kizazi chenye maadili na kinachochukia Rushwa, hivyo kusaidia kuongeza wigo wa kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Amesema, kutokana na ushirikishaji wa wanachi kupitia uelimishaji umma yamekuwepo matokeo chanya katika kuzuia vitendo vya rushwa na ubadhilifu nchini ambapo wananchi wamekuwa ni sehemu ya mafanikio ya vita ya rushwa na ufisadi kwa kuwafichua wanaojihusisha na vitendo hivyo, kutoa ushahidi mahakamani na kutambua wajibu wao wa kusimamia miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na Serikali.
UCHUNGUZI NA HUDUMA ZA SHERIA
Amesema, katika kipindi cha mwaka 2020/2021, kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi TAKUKURU imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi Billioni 29.3.
CP Hamduni amesema kuwa, TAKUKURU ilichunguza na kukamilisha majalada 1,053 ya makosa ya rushwa, yakiwemo majalada tisa (9) ya rushwa kubwa (uchunguzi unaohusisha thamani ya Shilingi bilioni 1 na zaidi) pamoja na majalada 28 yaliyotokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
"Kesi 503 ziliamuliwa mahakamani ambapo Jamhuri ilishinda kesi 347 sawa na asilimia 68.9 (68.9%) na kushindwa katika kesi 156 sawa na asilimia 31.1 (31.1%).
"Kesi mpya 544 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini zikiwemo kesi za Rushwa kubwa (Grand Corruption) nne (4), TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, imetaifisha mali zenye jumla ya thamani ya shilingi Bilioni 1.2 (1,217,000,000),"amesema.
Pia amefafanua kuwa, TAKUKURU imeweka zuio la fedha kiasi cha shilingi Milioni 495.5 (495,567,305.23) pamoja na mali zenye thamani ya shilingi Bilioni 2.6 (2,675,647,305.23), mali hizo ni pamoja na nyumba 15 katika maeneo mbalimbali nchini; viwanja viwili na magari matatu.
"Mheshimiwa Rais,Mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kupitia uchunguzi na huduma za Sheria kwa kuhakikisha mali zote zilizopatikana kwa njia za Rushwa zinataifishwa kwa mujibu wa Sheria.
"Aidha, tayari TAKUKURU imewasiliana na waajiri wa watumishi wa umma 257 waliokutwa na hatia mahakamani ili mamlaka za nidhamu za watumishi hao ziweze kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma,"amefafanua CP Hamduni.
USHIRIKIANO NA WADAU KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
CP Hamduni amesema kuwa, ni takwa la kifungu cha 4(2)(c) na 7(d) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, ambalo linaitaka TAKUKURU kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Amesema, katika kipindi cha mwaka 2020/2021, taasisi iliratibu na kusimamia utekelezaji wa Itifaki na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa za mapambano dhidi ya rushwa kwa kutambua kwamba Rushwa ni uhalifu mtambuka na mapambano yake yanahitaji ushirikiano na taasisi za nchi mbalimbali na Jumuiya za Kikanda za mapambano dhidi ya rushwa.
"Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa (United Nations Convention Against Corruption - UNCAC), pamoja na Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (African Union Convention on Preventing and Combating Corruption - AUCPCC).
"Taasisi kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Itifaki na mikataba ya kikanda na kimataifa ikiwemo,
"Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa, Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Shirikisho la Taasisi za Kupambana na Rushwa za Jumuiya ya Madola,Itifaki ya SADC ya Kupambana na Rushwa,Shirikisho la Taasisi za Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (Eastern Africa Association of Anti- Corruption Authorities EAAACA),"amefafanua CP Hamduni.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, kutokana na ushirikiano huo, wadau kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), chini ya Mradi wa Kujenga Uwezo wa Taasisi zinazosimamia Utawala Bora Awamu ya Tatu (Institutional Support for Good Governance ISPGG III),Action Aid,Konrad Adenauer Stiftung (KAS),
"Foreign Commonwealth Develepment Office (FCDO) chini ya Mpango wa Kujenga Uwezo Endelevu wa Mapambano Dhidi ya Rushwa nchini, yaani Building Sustainable Anti Corruption Action in Tanzania (BSAAT); pamoja na
"Women Fund Tanzania - Trust (WFT) chini ya Mradi wa Vunja Ukimya: Kataa Rushwa ya Ngono, waliendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa nchini kwa kupitia mafunzo, uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA, uelimishaji umma na ufuatiliaji wa fedha za umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,"amesema CP Hamduni.
Wakati huo huo, CP Hamduni amesema kuwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, inaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, "chini ya uongozi wako mahiri, kwa kusimamia mapambano dhidi ya rushwa kwa vitendo na kuiimarisha TAKUKURU katika nyanja zifuatazo:
RASILIMALI WATU
"Mheshimiwa Rais,katika eneo hili, watumishi 782 wa TAKUKURU wamepandishwa madaraja baada ya kukaa kwa muda mrefu katika daraja moja. Kibali cha kuajiri watumishi 350 kimetolewa, ili kuhakikisha kuwa TAKUKURU ina rasilimali watu inayokidhi mahitaji.
"Vilevile, tumepata kibali cha ajira mbadala kwa watumishi 51 ambao wamestaafu, wamefariki, wamefukuzwa kazi na kuacha kazi. Zaidi ya watumishi 400 wamepata mafunzo ya weledi ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na weledi,"amesema CP Hamduni.
Amefafanua kuwa, pamoja na Serikali kuiimarisha TAKUKURU katika nyanja ya Rasilimali Watu, pia imefanya jitihada kubwa za kuiimarisha TAKUKURU katika nyanja ya majengo
"Ujenzi wa ofisi ya TAKUKURU Makao Makuu Dodoma, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 20.8 (20,766,086,451.08). Mpaka sasa ujenzi wa msingi (Basement Floor), ghorofa ya chini (Ground Floor) pamoja na ujenzi wa nguzo za kupokea slab ya sakafu ya kwanza (First Floor), umekamilika na kazi ya ujenzi inaendelea.
"Mkandarasi wa jengo hili ni SUMAJKT CONSTRUCTION COMPANY LIMITED na Mshauri Elekezi ni Wakala wa Majengo Nchini Tanzania Building Agency (TBA),"amefafanua CP Hamduni.
Pia amesema, TAKUKURU imepokea kiasi cha Sh. Bilioni 1.5 kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Nyingine ni Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, uzio wa majengo ya TAKUKURU Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Wilaya ya Liwale mkoani Lindi pamoja na Ujenzi wa Karakana ya kutengeneza magari ya ofisi pamoja na Stoo makao Makuu Dodoma.
Sambamba na ukarabati wa jengo la TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Mkoa wa Morogoro pamoja na ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
KIWANGO CHA RUSHWA NCHINI KIMEPUNGUA
CP Hamduni amesema, juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya rushwa katika kipindi hiki nchini zimeleta mafanikio ambayo yanatambuliwa na Taasisi za Kimataifa.
Amesema, matokeo ya tafiti mbalimbali za kimataifa yanaonesha kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa.
TRANSPARENCY INTERNATIONAL
"Mheshimiwa Rais,taarifa ya Transperency International (TI) iliyotolewa Januari 2022, inaonesha kwa mwaka 2021 Tanzania imepata alama 39/100 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti.
"Haya ni mafanikio makubwa kwani tumepanda kwa nafasi saba ndani ya mwaka mmoja tu ukilinganisha na takwimu za mwaka 2020 ambapo Tanzania ilipata alama 38/100 na kushika nafasi ya 94 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti.
"Kulingana na taarifa hiyo ya Januari 2022, Tanzania imeshika nafasi ya pili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikitanguliwa na Rwanda,"amefafanua CP Hamduni.
WORLD JUSTICE PROJECT (WJP)
"Mheshimiwa Rais,Utafiti wa World Justice Project (WJP) inayotumia kiashiria cha The Rule of Law Index unaonesha kuwa kwa mwaka 2020, Tanzania iliendelea kufanya vizuri kwa mwaka wa pili mfululizo katika kukabiliana na vitendo vya rushwa hususan, katika kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka katika mihimili ya utawala, mahakama na bunge kwa kupata alama 0.47 na kushika nafasi ya 93 kati ya nchi 128 duniani, ikiwa ni nchi ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na nafasi ya 13 kwa nchi za chini ya jangwa la Sahara.
"Kulingana na kiashiria hiki, nchi inayopata alama 0 ina maana kwamba vitendo vya rushwa viko chini na usimamizi wa sheria ni madhubuti na nchi inayopata alama moja inaelezewa kuwa na udhahifu sana kwenye usimamizi wa sheria na imekithiri kwa rushwa.
"Mheshimiwa Rais,taarifa ya utafiti wa taasisi binafsi ya Research on Poverty Alleviation (REPOA), iliyotolewa mwezi huu (Machi 9, 2022), pia inaonesha kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kulikabili tatizo la rushwa, ambapo zaidi ya theluthi tatu (77%) ya Watanzania waliohojiwa, wamesema rushwa imepungua nchini katika kipindi cha miezi 12 iliyopita,"amefafanua CP Hamduni.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, mafanikio haya yanatokana na ushiriki wa wananchi, wadau na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita unayoiongoza katika kudhibiti vitendo vya rushwa nchini.
MWELEKEO WA TAASISI KWA MWAKA 2021/2022
CP Hamduni amesema kuwa, pamoja na jitihada kubwa ambazo zimeendelea kuchukuliwa katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, bado kuna changamoto ya uwepo ya vitendo hivyo hapa nchini.
Amesema, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, taasisi itaendelea kuzingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (Chama Tawala) ya Mwaka 2020 – 2025, Maelekezo ya Serikali na mipango mbalimbali ya Taifa katika kuwekeza nguvu kubwa za mapambano dhidi ya rushwa kwa kuzingatia vipaumbele mbalimbali.
KUZUIA
Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuzuia vitendo vya rushwa na ufisadi kabla ya kutokea kwa kufuatilia na kudhibiti mianya ya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi yote mikubwa ya kimkakati pamoja na matumizi ya fedha za UVIKO 19.
KUELIMISHA
Pia amesema, kipaumbele kingine ni kuelimisha wananchi na wadau kwa kutumia mbinu mbalimbali za uelimishaji ambazo zinalenga kuwahamasisha wananchi kushirikiana na Serikali katika kuzuia vitendo vya rushwa kabla havijatokea.
"Kufuatilia vitendo vya rushwa na kuchukua hatua stahiki katika; ununuzi wa umma, ukusanyaji wa mapato ya serikali pamoja na maeneo ya utoaji huduma muhimu kwa wananchi, kuimarisha ushirikiano wa wadau wengine wa ndani na nje ya nchi katika kuzuia na kupamba na vitendo vya rushwa,"amefafanua CP Hamduni."Mheshimiwa Rais kupitia hadhara hii, ninapenda kuwaomba watanzania wote hususani watumishi wa umma kutanguliza uzalendo na kuachana na vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo ni kikwazo kikubwa cha ukuaji wa uchumi imara wa Taifa letu.
"Mheshimiwa Rais,ulituelekeza kwenda kupitia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007 ili iweze kufanyiwa marekebisho iendane na mabadiliko ya sasa, ninapenda kukutaarifu kuwa maelekezo yako yametekelezwa na tayari sheria husika imepitiwa na maeneo yanayohitaji marekebisho ya kiutendaji na ya kisera yameainishwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS).
"Kwa sasa mapendekezo ya marekebisho husika yako kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua stahiki. Kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi wenzangu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wako mahiri, kwa utashi ulionao wa kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini.
"TAKUKURU inakuahidi kuwa itaendelea kuongeza juhudi katika kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye rasilimali za umma hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kabla havijatokeana kwa wale wote watakaobainika na kuthibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, Mheshimiwa Rais ninakuahidi hawatabaki salama,"amefafanua CP Hamduni.
KUHUSU TAKUKURU
TAKUKURU ni chombo cha umma chenye dhamana ya kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329.
Majukumu ya TAKUKURU ni pamoja na:kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa, wajibu wao wa kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na rushwa nchini.
Kufanya utafiti na uchambuzi wa mifumo ya utendaji na utoaji huduma katika sekta za umma na binafsi, wenye lengo la kubaini na kuziba mianya ya rushwa, kuishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya mapambano dhidi ya rushwa na kuchunguza tuhuma za makosa ya rushwa sambamba na kuwafikisha watuhumiwa wa vitendo vya rushwa mahakamani.
Tags
Habari
Kataa Rushwa
Rushwa ni Adui wa Haki
Rushwa ni Upofu
TAKUKURU
Tanzania Bila Rushwa Inawezekana