Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) laishauri jamii kuthamini na kuunga mkono juhudi za wanawake katika maendeleo

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara limeitaka jamii kuthamini na kuunga mkono juhudi za wanawake katika maendeleo mbalimbali wanayoyafanya kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa pia.
Hayo yamebainishwa Machi 8, 2022 na Afisa Mwelimishaji Jamii madhara ya Ukatili wa Kijinsia kutoka shirika hilo, Emmanuel Goodluck wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo katika Mkoa wa Mara yamefanyika Wilaya ya Butiama ambapo kwa mwaka huu yana kauli mbiu isemayo "Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu: tujitokeze kuhesabiwa".

Goodluck amesema kuwa, wanawake wameendelea kuonesha mchango wao mkubwa katika maendeleo kuanzia ngazi za familia, jamii na taifa katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana hivyo amesisitiza usawa uzidi kuzingatiwa katika ngazi mbalimbali ikiwemo kuwapa fursa za kuongoza, kuwashirikisha katika maamuzi, kumilikisha rasilimali kwa mendeleo endelevu ya jamii na taifa.
Pia, Goodluck ameitaka jamii kuondokana na mfumo dume ambao pia ni kikwazo katika maendeleo yao. Huku akisisitiza vitendo vya kuwakandamiza na kuwanyanyasa hasa maeneo ya vijijini viachwe kwani vinarudisha nyuma juhudi za kuleta usawa na maendeelo thabiti zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika.

Aidha,  Goodluck ameiomba Serikali kuendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo fursa za mikopo ili kuwajengea kujiamini na kumiliki rasilimali kwa ajili ya kupanua wigo wa maendeleo na usawa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
"Niombe pia madawati ya kijinsia yaendelee kuwapa elimu wanawake hasa maeneo ya vijijini. Wapo baadhi yao hawajui mambo mbalimbali zikiwemo haki zao pindi wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia, na wanawake kwa upande wao wayatumie madawati ya jinsia kupata elimu na ushauri chanya kwa manufaa yao na jamii pia," amesema Goodluck.

Ameongeza kuwa, Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) litaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali, wananchi na wadau mbalimbali kuweka msukumo chanya wa kusomesha watoto wa kike na kupigania haki na usawa sambamba na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake na aina nyingine za ukatili.
Debora Boniface ni Afisa miradi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ambapo amesema kuwa, shirika hilo pia limekuwa likiwaendeleza wasichana wanaokimbia aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kwa kuwaendeleza kielimu kwa wale wanaosoma wanaohifadhiwa Kituo cha Nyumba Salama Butiama na Mugumu vilivyopo chini ya shirika hilo.

Amesema, kwa upande wa wasichana ambao hawako katika mfumo rasmi wa elimu, shirika huwaendeleza katika stadi mbalimbali ikiwemo ushonaji ili wapate ujuzi na maarifa katika kuwajengea uwezo wa kujipatia kipato.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mara, Happiness Costantine amesema mabadiliko katika jamii yanaanza na wanawake wenyewe kujitambua, kujithamini, kujiheshimu na kutenda mambo mbalimbali ambayo yana faida kwao.
Ngariba mstaafu akikabidhiwa zawadi baada ya kuachana na ukeketaji. Katika picha ambayo anapokea.

Pia, amewataka wanawake mkoani humo kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ziweze kuwanufaisha na pia wajenge kujiamini na kushiriki katika masuala mbalimbali kwa manufaa yao.

Katika maadhimisho hayo, Ester Bhoke Mwita ambaye ni Ngariba mstaafu alikabidhiwa zawadi ya Shilingi 50,000. baada ya kuachana na kazi ya ukeketaji na kwa sasa ni balozi wa kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya vitendo hivyo kwa wasichana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news