Jaji Mkuu asisitiza matumizi ya TEHAMA

NA INNOCENT KANSHA-Mahakama Kuu

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema katika ziara yake Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea amehimiza sana matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na azma ya kuwa na Mahakama Mtandao katika ngazi zote za Mahakama ili kusogeza huduma karibu na wananchi hii itasaidia kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimuonyesha Kitabu cha utatuzi wa migogoro ya Ardhi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Pololet Mgema kilichoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), mara alipomtembelea Ofisini kwake Mjini Songea akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku nne kukagua shughuli mbalimbali za mahakama.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa kuhitimisha ziara yake ya kikazi Kanda ya Songea siku ya Machi 3, 2022, Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma alisema, Mahakama za Mkoa wa Ruvuma zimejitahidi katika matumizi ya TEHAMA hususani katika ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na ujazaji wa takwimu za mashauri kwa mtandao.

“Nimefarijika kuona majengo na viwanja vinavyomilikiwa na Mahakama vina hati miliki na vimewekwa katika mfumo wa kielekitroniki wa utambuzi wa majengo na mazingira yanayozunguka majengo (JMAP),”alisema Jaji Mkuu

Aidha, Prof Juma alisema, Mkoa wa Ruvuma una changamoto kubwa ya miundombinu ya Mahakama. Hali hiyo alijionea mwenyewe na imebainishwa pia na viongozi wa Serikali na wananchi wakati wa ziara hiyo. Ziara yake Mkoa wa Ruvuma ilimkumbusha kuwa, pamoja na hatua kubwa ambayo Mahakama imepiga katika maboresho ya miundombinu, mahitaji ya majengo ya Mahakama bado ni makubwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya songea wakati wa kufanya majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku nne (4) kukagua shughuli mbalimbali za mahakama Machi 3, 2022 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Kazi Songea

Mhe. Jaji Mkuu alitoa takwimu za Mkoa wa Ruvuma kuwa una jumla ya vituo vya Mahakama 54 vya ngazi mbalimbali kuanzia Mahakama Kuu (Songea), Mahakama ya Hakimu Mkazi (Songea), Mahakama za Wilaya 5 (Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru), na Mahakama za Mwanzo.

Kati ya vituo hivyo 54, ni majengo 15 tu ambayo hali yake inatajwa katika mipango ya Mahakama kuwa ni “nzuri”, na vituo 35 hali ya majengo yake imetajwa kuwa sio nzuri. “Yapo majengo ya Mahakama za Mwanzo yaliyofungwa kwa ajili ya uchakavu uliofikia hatua ya hatarishi kwa watumiaji. Kati ya Majengo 54, ni majengo 39 tu ndio yanamilikiwa na Mahakama, Majengo 15 ni ya kuazimwa kutoka Serikali za Mkoa, Wilaya, Kata, Vijiji au zinalipiwa pango kwa wanananchi. Kwa mfano, majengo yanayotumiwa na Mahakama ya Wilaya Songea, na Mahakama ya Mwanzo Songea Mjini, yameazimwa kutoka Sekreterieti ya Mkoa wa Ruvuma”, aliongeza Jaji Mkuu.

Kwa upande wa miundombinu ya Majengo nchini Jaji Mkuu, alisema Mahakama imejipanga kupunguza changamoto ya miundombinu ya majengo ya Mahakama kwa nchi nzima ikiwemo Mkoa wa Ruvuma.

“Tunao Mpango Mkakati wa Miundombinu na sasa tunauboresha ili kuzingatia uhalisia wa maeneo na changamoto mahususi za maeneo husika. Kwa mfano katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 mpango wetu ni kujenga maeneo yafuatayo ya mkoa wa Ruvuma,"amesema.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) mstari wa mbele akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma.

Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha kisasa hapa Songea kitakachokuwa na Mahakama ya Wilaya ya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Sehemu ya Mahakama ya Rufani. Aidha, kituo hicho kitakuwa pia na ofisi za Wadau muhimu wa utoaji wa huduma ya haki, pia tutajenga Mahakama ya Wilaya ya Nyasa na Mahakama za Mwanzo nne (4) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma”, alitoa ufafanuzi huo Jaji Mkuu.

Prof. Juma alisema, kwa ujumla, kuanzia mwaka ujao wa fedha yaani 2022/2023 Mahakama ya Tanzania inategemea kujenga majengo ya Mahakama za Mwanzo 60 kwa kutumia fedha za mradi wa Benki ya Dunia na majengo ya Mahakama za Mwanzo 10 yatajengwa katika maeneo magumu kufikika. Katika maeneo hayo kutajengwa jengo la Mahakama na nyumba za mahakimu.

Vile vile majengo ya Mahakama Kuu, Vituo Jumuishi 12 vitajengwa ambapo kati ya hivyo vituo 9 ni vya Mikoa isiyokuwa na Mahakama Kuu na vituo 3 ni Mikoa yenye Mahakama Kuu ambayo majengo yake ni chakavu na hayakidhi mahitaji muhimu ya kutolea huduma kama jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Songea, aliongeza Prof. Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) walioketi akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wa chama cha TAWJA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea.

Kwa upande mwingine Jaji Mkuu huyo alisema, Mahakama inatambua kuhusu upungufu mkubwa wa watumishi iliyonao. Mahitaji halisi ya watumishi ni takribani elfu kumi. Lakini watumishi waliopo ni takribani 5,830. Kwa Kanda ya Songea, mahitaji yao ya watumishi ni 336 lakini waliopo ni 179. Kwa hiyo kuna upungufu wa watumishi 157. Hivyo Mahakama itaendelea kushirikiana na Serikali kutatua changamoto hiyo kwa awamu.

Jaji Mkuu alitolea mfano kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mahakama imeajiri watumishi 340. Ni lengo la Mahakama pia mwaka ujao wa fedha itapata kibali cha ajira mpya kutoka Serikalini.

“Kwa sababu hizo Mahakama inasisitiza matumizi ya TEHAMA kama namna moja wapo ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi. Tunahimiza pia watumishi kujiendeleza kusoma taaluma zaidi ya moja (multi skilled personnel) ili waweze kufanya kazi kwa tija kubwa,” alisema.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) walioketi akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea.

Amesema kuwa kuna uboreshaji mkubwa unaofanyika ndani ya Mahakama kama ilivyo kwa upande wa Serikali na Bunge. Hata hivyo, amebainisha kuwa pamoja na maboresho ya miundombinu, Mahakama inasisitiza mabadiliko ya mitazamo na fikra chanya kwa watumishi wa Mahakama na wadau wetu. Amesma watumishi na wadau wakiwa na fikra chanya na kufikiri kimkakati, changamoto kwenye mnyororo wa utoaji haki zitatatuliwa kwa uharaka na hatimaye wananchi kupata huduma zilizo bora.

“Mahakama imejipanga kuendelea kuboresha usikilizaji wa mashauri kwa lengo la kumaliza mashauri kwa wakati. Kwa Kanda ya Songea kasi ya usikilizaji wa mashauri ni nzuri na kwa asilimia kubwa wamefikia malengo ya kumaliza mashauri. Yako mashauri machache yalibaki mwaka jana lakini ni kutokana na sababu zilizo nje ya Mahakama kama mashahidi kutofika mahakamani na upelelezi kutokamilika mapema. Tutawasiliana na wenzetu ili kuondoa changamoto hii ambayo inaweza kuchelewesha haki kutolewa,”amesema.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama pia imeweka mipango madhubuti ya kusikiliza kwa haraka mashauri ya Mirathi na Ndoa. Amesema katika eneo hilo wanaoathirika sana ni wanawake na watoto, hivyo watafanya kila linalowezekana kuhakikisha mashuri ya mirathi na ndoa yanamalizika mapema.

Kwa sababu hiyo tumeanzisha kituo jumuishi cha masuala ya Mirathi na Ndoa pale Temeke. (kama Pilot Centre). Tutakachojifunza katika kituo hiki kitasaidia kuenezwa sehemu zingine hapa nchini,” amesema.

Mhe. Prof. Juma amesema pia kuwa katika ziara ya Mkoa wa Ruvuma amepata fursa ya kuona uhalisia wa mazingira ya kutolea haki ikiwemo miundombinu ya majengo, ukubwa wa maeneo yanayohudumiwa na Mahakimu na umbali wa vituo vya kutolea haki.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) walioketi akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wa chama cha JMAT wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea. (Picha na Innocent Kansha - Mahakama).

“Nimepokea maoni na mapendekezo ya wadau wetu kuhusu utendaji wa kazi za Mahakama na maoni yao ya namna ya kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa haki. Nimefariji kwa maoni na mapendekezo yao. Niliwaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Yale yanayohusu Mhimili wa Utawala (Serikali) tutayawasilisha kwa wahusika na naamini watayafanyia kazi,”amesema.

Aidha, Jaji Mkuu alibainisha kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa na uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Serikali ili kutatua changamoto ya uchache wa watumishi kadri bajeti itakavyoruhusu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news