NA MWANDISHI DIRAMAKIN
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya ujambazi na unyang'anyi wa kutuma silaha.Kamanda wa Polisi katika kanda hiyo, ACP Muliro Muliro ameyasema hayo leo Machi 22, 2022 wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Amesema, watuhumiwa hao wamewakamata kufuatia kufanya muendelezo wa operesheni kali iliyoanza tangu Machi 16,2022 hadi Machi 20,2022.
Kamanda Muliro amesema, watu hao huwa wanatumia pikipiki kutekeleza matukio hayo ya kihalifu katika jiji la Dar es Salaam ambapo amewataja ni pamoja nja Mussa Abdulrashid (28) mkazi wa Vikindu na Tuangoma Temeke na Erick Joseph Mfuko (32) mkazi wa Kibamba.
Aidha, Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bunduki aina ya Pistol mbili Browning namba za usajili TZCAR 113805 na Glock 15 nambari TZCAR 9611 zikiwa na risasi sita kwenye Magazine pia Pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 123 DAL ambayo wamekuwa wakiitumia kufanya uhalifu imekamatwa.
"Watuhumiwa hawa wamekiri kuhusika na matukio mbalimbali tangu mwaka 2021 kwa kuwafuatilia kwa nyuma na pikipiki yao baadhi ya watu waliochukua pesa zao kutoka benki ya CRDB Kibada, CRDB Pugu Road, NMB Banana, CRDB Temeke, NMB Airport na Kampuni ya ASAS zote za Dar es Salaam,"amesema Kamanda Muliro.
Pia amesema, mmoja wa watuhumiwa hao mwaka 2018 amewahi kukamatwa na kupelekwa mahakamani na gerezani kwa tuhuma za unyang’anyi.
Kamanda Muliro amesema, baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa wamekiri kuhusika na matukio hayo na mahojiano kwa kina bado yanaendelea ambapo pia ametoa onyo kwa mtu au vikundi vya watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja.
Amesema, Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwakamata pia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.Wakati huo huo,jeshi hilo limewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu pindi wanapowabaini kwenye maeneo yao ili waweze kudhibitiwa kwa wakati.