Kamati ya Bunge yapitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini 2022/2023

*Waziri Biteko aahidi matokeo chanya

NA MWANDISHI MAALUM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo Machi 29, 2022, imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Kamati hiyo imepitisha makadirio hayo baada ya awali kupokea taarifa za utekelezaji wa bajeti ya wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Februari 2022.
Katika mawasilisho hayo, kamati ilionesha kuridhishwa na mwenendo mzuri wa makusanyo ya wizara, maendeleo ya Sekta ya Madini, kasi ya ukuaji wa sekta pamoja na utekelezaji wa majukumu na miradi mbalimbali inayosimamiwa na wizara na taasisi zake.
Baada ya wizara kuwasilisha taarifa za utekelezaji, pia, iliwasilisha kwa kamati hiyo makadirio ya mapato na matumizi ya wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 ambapo kamati hiyo imeyapitisha katika kikao kilichofanyika leo jijini Dodoma.
Akizungumza katika Kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dunstan Kitandula amesisitiza wizara kuangalia namna bora itayowezesha usimamizi wa matumizi ya fedha zinazotolewa na kampuni kubwa zinazofanya shughuli za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kwamba, fedha hizo zinaleta tija katika maeneo yanayozunguka migodi hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameihakikishia kamati kulifanyia kazi suala hilo na kutumia fursa hiyo kuwataka wajumbe wa kamati hiyo walioko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka katika maeneo ambayo yanafanya vizuri katika matumizi ya fedha hizo.

“Nampongeza Mhe. Musukuma amechangia kwa kiasi kikubwa kuleta mageuzi katika masuala ya fedha za CSR ni vizuri wabunge wengine mkabadilishana uzoefu. Kwa upande wetu kama sekta tunakwenda vizuri hata nchi nyingine wanakuja kwetu kujifunza,’’amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ameishukuru kamati hiyo kutokana na ushauri inaoipatia wizara ambao umewezesha wizara kujisahihisha na hivyo kuiwezesha kujipima namna inavyosimamia na kutekeleza Sera na Sheria na kueleza kuwa, kama wizara itajitahidi kutopindisha maelekezo ya kamati.
“Tunashukuru sasa wajumbe wanaielewa sekta, wanatupatia uzoefu wa wenzetu kutuwezesha kufanya vizuri, tunashukuru kamati kutupitishia bajeti hii, tunapenda fedha yote tunayoipata iwe na matokeo mazuri,’’amesisitiza Dkt. Biteko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news