Kamati ya Bunge yashuhudia kazi kubwa inayofanywa na TAEC ujenzi wa Maabara Changamana jijini Arusha

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa hatua kubwa iliyofikia katika ujenzi wa mradi wa Maabara Changamana Awamu ya Pili (Mradi Namba 6352) ambapo mpaka kufikia leo Machi 15, 2022 utekelezaji wake umefikia asilimia 94 ili kukamilika.Pongezi hizo zimetolewa leo, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya kufanya ziara Makao Makuu ya TAEC jijini Arusha ili kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa mradi wa Maabara Changamana awamu ya pili unaojengwa na Serikali kwa jumla ya Shilingi Billioni 10.4.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza ufanisi zaidi kwa tume hiyo katika kutekeleza majukumu yake ambayo yameendelea kuwa na matokeo makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) iliundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003).Sheria ya Bunge Na. 7(2003) ilifuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).

Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Ni kutokana na ukweli kwamba, teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, kilimo, ufugaji, viwanda, maji na utafiti.

TAEC imepewa jukumu la kupima mionzi kutokana na sababu mbalimbali, kwani licha ya kuwa na faida nyingi za mionzi, isipotumika inavyotakiwa ni hatari ikiingia katika mnyororo wa chakula kwa sababu inatoa nishati toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile.
Kwa mujibu wa tume hiyo, viasili vya mionzi vinaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama. Hivyo, sababu kuu za kupima mionzi katika mnyororo wa chakula ni kuhakikisha chakula kinacholiwa na Watanzania hakina mionzi na hivyo kuwa salama kwa matumizi ya kawaida.

Pia ni muhimu kuhakikisha kuwa soko la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinalindwa ili kuzingatia ubora na viwango vilivyowekwa kulingana na miongozo na taratibu mbalimbali za Serikali.
Miongoni mwa sababu zinazosababisha upimaji wa mionzi ni kutokana na ukweli kuwa, usafirishaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking) unaweza kusababisha uchafuzi kwenye vyakula na mazingira.

Sababu nyingine kwa mujibu wa TAEC ni kuwepo kwa mionzi asili kwenye udongo na mazingira yetu kama vile madini ya urani katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia kila mmoja wetu anatambua kuwa, ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi, hivyo kupitia tume hiyo imechukua hatua za kulinda mnyororo mzima wa chakula ili wananchi wake wawe salama
Sambamba na kulinda soko la bidhaa zetu zinazouzwa nje ya Tanzania hasa wakati huu wa vita ya kiuchumi. Upimaji unatoa uwezekano wa kufuatilia kama kuna shida yoyote ikiewemo kutekeleza takwa la kisheria, kupima mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama ilivyoahinishwa kwenye Sheria Na. 7 ya Mwaka 2003.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news